NA OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amewaagiza Waganga Wakuu Wa Mikoa kusimima nidhamu ya watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya msingi ikiwemo kutumia lugha mbaya na isiyo rafiki kwa wagojwa wakati wa utoaji huduma.
Bashungwa ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma katika kikao cha kujadili utekelezaji wa Mkataba wa afua za lishe nchini kilichowashirikisha Waganga wakuu wa Mikoa, Maafisa lishe wa Mkoa na wadau wa lishe Mei 26, 2022 amesema, alipokuwa mkoa Mara alikutana na kero za wananchi wakilalamikia baadhi ya wahudumu wa afya kutumia lugha chafu kwa wagonjwa.
“Kwenye ziara zangu nimekuwa nikikumbana na kero za wananchi wakati wakipatiwa huduma ikiwemo kauli zisizo rafiki kwa baadhi ya Wauguzi kwa wagojwa na nitumie nafasi hii kuwaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa kuendelea kusimamia nidhamu ya watumishi katika vituo vyetu vya kutolea huduma,” amesema Bashungwa.
Bashugwa ameeleza kumekuwepo na changamoto ya kutopatikana kwa baadhi ya madawa ya kutosha ambapo Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wanaendelea kufuatilia na kuhakikisha fedha zilizopelekwa Wizara ya afya kupitia MSD yanapatikana madawa ya kutosha katika vituo vyote vya huduma za afya.
Aidha, amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa kuendelea kusimamia sehemu yao na kukwamua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosuasua katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa Watanzania.
