PETER HAULE NA SAIDINA MSANGI-WFM
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, (Mb) ametoa rai kwa sekta binafsi nchini kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo ili kutoa nafasi kwa Serikali kutoa huduma kwenye maeneo ambayo sekta binafsi haiwezi kufika.Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiongoza kikao kati yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABSA Afrika, Bw. Saviour Chibiya, jijini Dodoma.
Alitoa rai hiyo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABSA Afrika, Bw. Saviour Chibiya ambaye Benki yake inamiliki zaidi ya asilimia 50 ya hisa za Benki ya NBC.
Alisema kuwa muelekeo wa Serikali ni kuwa kazi zinazoweza kufanywa na sekta binafsi ziweze kufanywa na sekta hiyo kwa sababu kadri sekta hiyo inavyokuwa ndivyo inavyotengeneza ajira kwa vijana.
Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Japhet Justine, akizungumza jambo wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABSA Afrika, Bw. Saviour Chibiya (wa kwanza kulia), jijini Dodoma.
“Sasa hivi Serikali inajenga Reli ya Kisasa lakini inakaribisha Sekta binafsi katika masuala ya uendeshaji na mengine yanayoweza kufanywa na sekta hiyo, mpaka sasa miongoni mwa mambo ambayo sekta binafsi imeshirikiana na Serikali katika suala hilo ni pamoja na kuleta vichwa vya treni na mabehewa jambo ambalo linatakiwa lifanyike katika sekta nyingine pia,’’ alisema Dkt. Nchemba.
Akieleza kuhusu sekta ya kilimo, Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali inatarajia kuanzisha miradi ya kilimo cha umwagiliaji na inatarajia kuona sekta binafsi hasa benki ikishiriki kikamilifu katika kuwawezesha wakulima hususani walio katika vikundi kwa kuwapa mikopo itakayowasaidia kupata mitaji ili waweze kuingia katika shughuli za uzalishaji.
Dkt. Nchemba aliongeza kuwa Sekta zingine ambazo zinahitaji kwa kiasi
kikubwa uwezeshaji kutoka sekta binafsi ni pamoja na uvuvi na ufugaji
kwa kuwa ni maeneo ambayo yanaweza kuwa suluhisho la changamoto ya
upatikanaji wa ajira kwa vijana.
Aidha, alipongeza benki hiyo kwa
kuunga mkono sekta ya michezo kwa kudhamini ligi kuu ya Tanzania bara
ambapo udhamini huo umechochea hamasa ya mchezo wa mpira wa miguu
nchini.
Alitoa rai kwa benki hiyo kuendelea kuunga mkono Serikali
katika sekta nyingine ikiwemo sekta ya afya ambapo, Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan, amejenga vituo vingi vya afya ambavyo vinahitaji vifaa
tiba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABSA Afrika, Bw. Saviour Chibiya, aliipongeza Serikali kwa jitihada za kukuza uchumi licha ya changamoto ya Uviko 19 pamoja na vita ya Urusi na Ukraine, jambo ambalo alilitaja kuwa ni kichocheo kikubwa cha uwekezaji.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (wa pili kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya ABSA Afrika Bw. Saviour Chibiya (wa pili kushoto), Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa, Bw. Japhet Justine (wa kwanza kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw. Theobald Sabi, wakiwa katika picha ya pamoja, baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao uliofanyika, jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Srikalini, WFM, Dodoma).
Alisema kuimarika kwa uchumi kunawafanya wawekezaji ikiwemo Benki ya ABSA Afrika kuvutiwa kuwekeza Tanzania, hivyo benki yake ipotayari kuendelea kuwekeza nchini ili kuchochea maendeleo ya jamii kwa kuwa uwekezaji ni miongoni mwa jukumu lao muhimu.