Waziri Mkuu: Watanzania tusishawishike kudharau vya kwetu, tusimame pamoja kutangaza vivutio vyetu, Royal Tour inalipa

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuitangaza kwa bidii filamu ya Royal Tour pamoja na vivutio mbalimbali vilivyoko nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi walioshiriki katika uzinduzi wa filamu ya The Tanzania Royal Tour katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma,Mei 15, 2022. Kutoka kushoto ni Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Ninawasihi Watanzania tusishawishike kudharau vya kwetu, tusimame pamoja kutangaza vivutio vyetu na kupitia utalii huu, tutafungua ajira kwa waongoza utalii na kada nyinginezo,” amesema.

Ametoa wito huo usiku wa Mei 15, 2022 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali na mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma waliofika kushuhudia uzinduzi wa filamu hiyo, kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

“Baada ya hapa, wana Dodoma twende tukaisemee filamu hii kwa kutumia simu zetu na mitandao ya kijamii,” amesema Waziri Mkuu ambaye alikuwa akimwakilisha Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango.

Amesema kuzinduliwa kwa filamu ya Royal Tour kumefungua zaidi milango ya utalii na kwani baada tu ya uzinduzi Tanzania ilipokea watalii 796 kutoka Israeli ambao walikuja kwa ndege tatu zilizofuatana.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka Wakuu wengine wa Mikoa watenge siku moja na kuwashirikisha wananchi wao washuhudie kazi kubwa ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais.

“Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Mtaka yeye kaanza. Ni vema Wakuu wengine wa Mikoa watafute siku moja ya kuwaonesha watu wao, wanaweza kuchagua hata kwenye ngazi ya Halmashauri ili waone juhudi za Mheshimiwa Rais wetu,” amesisitiza.

Amesema kitendo cha Mheshimiwa Rais Samia kuruka kwa ndege na kuonesha kwa karibu kilele cha Mlima Kilimanjaro, kimekata mzizi wa fitna juu ya mahali halisi ulipo mlima huo. “Mheshimiwa Rais amekata mzizi wa fitina na kuithibitishia dunia kuwa Mlima Kilimanjaro uko Tanzania.” Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi kwa naiba ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka Kwenye uzinduzi wa filamu ya The Tanzania Royal Tour uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akielezea fursa zilizopo kwenye mkoa wa Dodoma, Waziri Mkuu ametaja kilimo cha zabibu, usindikaji wa mvinyo, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), eneo la kuandaa wapigania uhuru wa Namibia, Angola, Afrika Kusini, Zimbabwe na Msumbiji, mapori ya akiba ya wanyamapori ya Mkungunero na Swagaswaga na mazalio ya wanyama ya hifadhi ya Tarangire kama baadhi ya vitu vinavyoweza kuuinua mkoa huo.

“Uendelezaji wa vivutio hivi utawafanya wakazi wa Dodoma wapate mahali pa kupumzikia, nawasihi wawekezaji waje Dodoma sababu ni mahali sahihi kwa uwekezaji na utalii.”

“Si hivyo tu, fimbo ya Mtemi Mazengo iko Dodoma, baiskeli yake aliyotumia iko Dodoma, kaburi lake liko Dodoma na pia nyumba ya kuhifadhi madini iliyojengwa mwaka 1925. Ninatoa wito kwa Bodi ya Utalii ishirikiane na uongozi wa Mkoa wa Dodoma ili kuhifadhi vivutio hivi.” 

Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas alisema matarajio ya awali yalikuwa kuwafikia watu bilioni moja lakini kutokana na tafiti za kisasa, matarajio ya sasa ni kuwafikia watu bilioni mbili.

Alisema filamu ya Royal Tour ni fursa ya pekee ya kuitangaza Tanzania, ni fursa ya kutandaa duniani (networking) kwani imemuwezesha Mheshimiwa Rais kukutana na wafanyabiashara maarufu na wamiliki maarufu wa makampuni makubwa duniani ya utalii, filamu, meli za utalii na mahoteli maarufu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news