Waziri Mkuu:Timu ya Mawaziri nane inahusika na migogoro mikubwa tu

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema timu ya mawaziri nane kutoka wizara shiriki inashughulikia migogoro mikubwa tu ya ardhi ambayo hulazimu kukutanisha wataalamu kutoka wizara husika.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali bungeni jijini Dodoma, Mei 19, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa kauli hiyo leo Mei 19, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbarali, Bw. Francis Mtega kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye aliuliza ni kwa nini baadhi ya maeneo yenye migogoro nchini hayajajumuishwa kwenye Kamati ya Mawaziri nane wa sekta husika.

“Migogoro hii ina ngazi mbalimbali za utatuzi na sisi Serikali tumeweka utaratibu. Kwanza, migogoro yote ya ardhi, inaratibiwa katika ngazi ya kijiji, na hii kamati ya kijiji inaweza kutatua migogoro kwa kukutanisha wenye migogoro. Baada ya hapo inaenda ngazi ya kata, wilaya na kisha ngazi ya mkoa.”

Amesema Kamati ya Mawaziri nane imeendelea kufanya kazi ya kubainisha maeneo tangu mwaka 2019 na tayari ilishapeleka taarifa Bungeni ya vijiji vilivyofikiwa na kubainisha vijiji vilivyokuwa na migogoro.

“Taarifa ilibainisha maeneo ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji, wakulima na maeneo ya hifadhi. Kamati ya Mawaziri inaendelea kubaini maeneo yenye migogoro yenye tija na yasiyo na tija ili kila mmoja aendelee kufanya kazi yake, iwe ni ufugaji, kilimo au uvuvi. Pindi kazi hiyo ikikamilika, tutatoa taarifa ili Waheshimiwa Wabunge muwe na taarifa ya maeneo yenu,” amesema.

Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeridhia maeneo ya hifadhi yasiyo na tija na imeruhusu wananchi waendelee kufanya kazi zao.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutoa ruzuku kwenye mazao yanayolimwa nchini kulingana na uhitaji uliopo na aina ya mazao.

“Upo mkakati wa Serikali wa kutoa ruzuku kwa mazao mbalimbali ikiwemo kahawa kutegemea na aina ya mazao husika. Ruzuku inategemea aina ya zao na mahitaji yake makubwa. Kuna mahitaji ya miche, dawa, mbegu, mbolea au ya maghala,” amesema.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Esther Malleko ambaye alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa zao la kahawa linapatiwa ruzuku kwa vile halijawahi kuwekewa ruzuku ikilinganishwa na mazao mengine ya kimkakati.

“Juzi nilikuwa Bukoba kwenye kikao na wadau wa zao hilo. Kule wanahitaji zaidi miche na vyama vikuu vya msingi walisema wana upungufu wa maghala. Niliwahi kwenda Mbinga, wao wanahitaji zaidi mbolea kwa sababu kule bila mbolea, huwezi kukuza zao hilo.”

Waziri Mkuu amesema Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akihitimisha bajeti ya wizara yake, ameahidi kujenga maghala 300 kule Kagera kwa sababu tunajiandaa kuingia kwenye mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani na bila maghala kuwepo huwezo kutumia mfumo huo.

Amemuahidi mbunge huyo kuwa ikifika zamu ya ruzuku kwa mkoa wa Kilimanjaro, yataangaliwa kwanza mahitaji yao ni yapi na utaangaliwa mpango wa Serikali kutoa ruzuku ukoje ili kuona kama unaendana na mahitaji yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news