Yanga SC wazidi kuitibua Simba SC Ligi Kuu ya NBC

NA DIRAMAKINI

MABINGWA watetezi, Simba SC wametoa sare ya bila mabao na vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kupitia Derby ya Kariakoo.
Ni mtanange wa aina yake ambao umepigwa Aprili 30, 2022 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Beki Henock Inonga Baka (Varane) wa Simba na mshambuliaji, Fiston Kalala Mayele wa Yanga ndiyo walioonekana kunogesha mtanange huo kwa namna ambavyo wamepambana dimbani.

Aidha, kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza ya ligi, Inonga alimdhibti vyema Mayele, kinara wa mabao Ligi Kuu ambaye muda wote wa mchezo alipiga shuti moja tu lililogonga nyavu za pembeni, nje kulia kipindi cha pili.

Simba SC pekee waliofanya jaribio la hatari lililolenga lango,ni baada ya mshambuliaji Chris Kope Mutshimba Mugalu kuunganishia mikononi mwa kipa Djigui Diarra mpira wa adhabu wa beki Shomari Kapombe kipindi cha pili pia.

Pia mtanange huo ulikuwa wa kukamiana na kuonyeshana ubabe baina ya wachezaji wa pande zote mbili.

Refa chipukizi, Ramadhani Kayoko alionekana kuumudu vilivyo mtanange huo licha ya makosa machache ya kibinadamu aliyoyafanya.

Simba SC kwa sare hiyo wanafikisha alama 42 baada ya mechi 20, wakizidiwa alama 13 na watani wao wa jadi, Yanga ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi.

Aidha, watani hao wa jadi wanaweza kukutana tena kabla msimu kufungwa katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), iwapo Simba wataitoa Pamba FC ya Mwanza.

Pengine huu unaweza kusema ulikuwa ni mchezo mkali wa mzunguko wa pili na kufanya dakika 180 kukamilika bila kufungana.
Ule wa awali,ubao ulisoma Simba 0-0 Yanga hivyo katika msako wa alama sita watani hao wamegawana alama mbili mbili.

Utabiri wabuma

Hassan Bumbuli,Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wanaamini wanaweza kuwafunga wapinzani wao wa leo na kuodoka na pointi tatu muhimu. 

“Kama itakuwa hivi ninadhani labda itakuwa wenyeji 2, (Yanga) na wao 0, (Simba) kwenye mchezo wetu wa dabi ambao utachezwa Uwanja wa Mkapa. Wakijitahidi sana kwenye mchezo wetu labda itakuwa 2-1 ila ambacho ninajua ni kwamba tunakwenda kwenye mchezo tukiamini kwamba tunacheza na timu kubwa na yenye wachezaji wazuri,”amesema Bumbuli awali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news