NA DIRAMAKINI
TIMU ya Tanzania Prisons imechapwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Wenyeji hao wamepoteza fursa hiyo wakiwa katika dimba la Sokoine jijini Mbeya kupitia mtanange uliopigwa leo Mei 16,2022.
Bao pekee la Kagera Sugar katika mchezo wa leo limefungwa na beki mkongwe, David Luhende dakika ya 88.
Kwa ushindi huo, wanafikisha alama 32 na kusogea nafasi ya tano, wakati Tanzania Prisons inabaki na alama zake 23 nafasi ya 15 baada ya wote kucheza mechi 24.
Wakati huo huo, wenyeji Ruvu Shooting wamelazimishwa sare ya 1-1 na KMC Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani.
Awali Ruvu walitangulia na bao la mshambuliaji wake mkongwe, Fully Zulu Maganga dakika ya 19, kabla ya kiungo Awesu Awesu kuisawazishia KMC dakika ya 88.
Kwa matokeo hayo,Ruvu wanafikisha alama 26 nafasi ya 13 na KMC sasa wana alama 28 nafasi ya nane baada ya wote kucheza mechi 24.
Jumla ya timu 16 zinashiriki Ligi Kuu na mwisho wa msimu mbili zitateremka moja kwa moja na mbili zitakwenda kumenyana na timu za Championship kuwania kubaki Ligi Kuu ya NBC.
Mei 15,2022 Yanga SC walizidi kujiongezea nafasi ya kulitwaa taji la Ligi Kuu ya NBC kwa msimu huu baada ya kujinyakulia alama tatu.
Ni alama tatu ambazo zilisindikizwa na mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara uliopigwa katika dimba la Jamhuri jijini Dodoma.
Ushindi huo wa kwanza katika mechi nne ulitokana na mabao ya kiungo Dickson Ambundo dakika ya 11 akiiadhibu timu yake ya zamani na kipa Mohamed Yussuf aliyeudondeshea mpira langoni mwake katika harakati za kuokoa shuti la Zawadi Mauya dakika ya 35.
Wanajangwani wanafikisha alama 60 katika mechi ya 24 na kuendelea kuongoza ligi kwa alama 11 zaidi ya mabingwa watetezi, Simba ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi.