NA FRESHA KINASA
MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Health Environment Community Empowerment and Development in Tanzania (HECEDET) ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa la New Life Gospel Community Church -Tanzania (Bonde la Baraka) nchini lenye Makao Makuu yake Kigera Bondeni Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara, Daniel Ouma amesema, ili kuendelea kuwa na mazingira bora ya kijani na endelevu wazazi na walezi wawajibike kuwapa jukumu watoto wao la upandaji wa miti na kuwafundisha jinsi ya kuiendeleza kuanzia katika familia zao.
Amesema, hatua hiyo itawafanya wawe mabalozi wema na thabiti wa mazingira wakiwa katika umri mdogo na kwamba wakifikia umri wa miaka 18 na kuendelea watazidi kuendelea kuwa mabalozi wa kutunza mazingira pamoja na uoto wa asili kutokana na msingi bora waliojengewa kuanzia utotoni.
Askofu Ouma ameyasema hayo leo Juni 3, 2022 wakati akiongoza zoezi la upandaji wa miti katika Shule ya Msingi Mwembeni 'A' na 'B' zilizopo Manispaa ya Musoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambayo huadhimishwa Juni 5 kila mwaka.
Amesisitiza, wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi za serikali katika utunzaji wa mazingira ikiwemo kupanda miti katika maeneo yao, kufanya usafi wa mazingira na kutoharibu uoto wa asili kwa kufanya shughuli za kibinadamu ambazo si rafiki kwa mazingira.
"Hatuwezi kuwa na afya bora pasipo kuwa na mazingira bora, ili kuwa na watu makini ambao ni wachapakazi na wazalishaji lazima wathamini faida na thamani ya kuishi katika mazingira Safi, Salama na yenye kuwezesha shughuli za maendeleo kufanyika kwa ufanisi. Niwahimize Wazazi na walezi pamoja na jamii, mkazo uwekwe katika kuwajenga watoto kutunza mazingira wakiwa nyumbani na ikibidi mtoto apewe mti ausimamie vyema uweze kukua na katika taasisi za elimu (shuleni au vyuoni) wawe na miti ambayo wataisimamia chini ya uangalizi wa walimu,"amesema Askofi Ouma.
Ameongeza kuwa, Shirika la HECEDET kwa sasa linatekeleza Mradi wa Tunza Mazingira Yangu' mkoani wa Mara ambapo shabaha ni kuhakikisha mazingira yanakuwa na mchango katika kufanikisha maendeleo na kuunga mkono juhudi za serikali kwa kupitia uratibu, uwezeshaji, uhamasishaji, utekelezaji, tathmini, ufuatiliaji na tafiti za kimazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la HECEDET Mkoa wa Mara, Odilia Damas amesema, miti mingi imekuwa ikipandwa lakini hushindwa kukua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo watu kutokuwa na elimu ya upandaji wa miti, kutopanda mti katika eneo rafiki pamoja na imani potofu kwa baadhi ya watu kwamba baadhi ya miti ikipandwa katika familia zao huleta mikosi na kuchangia vifo jambo ambalo halina ukweli ndani yake.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwembeni ' B', Francis Magesa ameshukuru hatua ya Askofu Ouma kuonesha upekee katika suala zima la utunzaji wa mazingira na ushiriki wake wa dhati katika kupanda miti katika shule hiyo sambamba na utoaji wa elimu ya mazingira kwa wanafunzi wa Shule hiyo kupitia Shirika la HECEDET ambalo limekuwa mstari wa mbele katika suala zima la uhamasishaji wa kutunza mazingira .
"Elimu hii ya mazingira inayotolewa kwa wanafunzi wa Shule zetu za msingi yaani Mwembeni 'A' na 'B' inamanufaa makubwa sana hasa katika kuwajenga wanafunzi kupenda kutunza mazingira na kutambua faida, na madhara ya kutotunza mazingira naamini watatoa hamasa na msisitizo na pia watakuwa mabalozi wa mazingira kwa sasa na siku za usoni,"amesema Mwalimu Magesa.