NA DIRAMAKINI
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limetoa rai kwa Watanzania wote kujiandaa kushiriki kikamifu kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika mwezi Agosti 23, mwaka huu kwa ajili ya kuiwezesha Serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.
Katibu Mkuu wa BAKWATA Tanzania,Alhaj Nuhu Mruma amesema, "Nichukue nafasi hii kuwahimiza Watanzania, Waislamu na wasiokuwa Waislamu tuko katika maandalizi ya zoezi muhimu la kitaifa la Sensa ya Watu na Makazi. Kama tulivyoambiwa na vyombo vinavyosimamia sensa, sensa hii itafanyika Agosti 23 mwaka huu na maanndalizi yote yamekamilika.
"Nafasi yetu kama viongozi wa dini na wengine ni kuhimiza wananchi wote siku hiyo ikifika kwenda kuhesabiwa kwa sababu sensa kwa mujibu wa dini yetu ni jambo zuri. Tunaunga mkono mambo yote ambayo yanafanywa na Serikali hayana mushikeli, tunayaunga mkono na kuyapa kipaumbele. Kwa hiyo tunatoa wito kwa Waislamu wote, wananchi wote kuwapa ushirikiano maafisa na makarani wa sensa ifikapo tarehe hiyo 23 Agosti mwaka huu.
"Lakini pia tuhakikishe kwamba katika majukwaa yetu mbalimbali katika hadhara zetu zote swala zetu za Ijumaa tunawahimiza watu kuhusu umuhimu wa sensa. Sensa ni muhimu katika nchi kwa sababu inatoa takwimu zitakazoisaidia nchi katika kuandaa mipango mbalimbali ya maendeleo, mipango ya miundombinu, elimu, dawa, afya na kadhalika bila kuwa na takwimu hizo huwezi kujua unaweza kutoa huduma hizo kwa namna gani.
"Kwa hiyo, ukikataa kuhesabiwa umejinyima wewe mwenyewe fursa ya kupatiwa huduma pale ulipo wewe, asiwepo mmoja yeyote atakayeachwa kuhesabiwa. Sensa kwa maendeleo tujiandae kuhesabiwa.
"BAKWATA makao makuu kupitia mheshimiwa Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania tumeshatoa wito, Mufti ameshatoa na mimi nimesharudia mara nyingi kwa hiyo viongozi wa mikoa yote lichukulieni hili jambo kama agizo kulishusha kuanzia ngazi ya mikoa, wilaya kata hadi msikitini kwa wale Maimamu na Makatibu wa swala za Ijumaa tuwaelimishe wananchi kuhusu sensa." amesema.
"Hili ni agizo kutoka juu kwamba tuifanyie kazi hii sensa, wanasema kadhia iliyopo sasa (current issue) ni sensa tuifanyie kazi, tuelimishe na tuifanyie kazi na tutoe nafasi kwa wengine katika ngazi zingine waweze kufanya maamuzi kwa ajili ya maendeleo,"amesema.