NA DIRAMAKINI
BENKI ya Letshego Tanzania wamezindua rasmi aina mbili za mikopo ambayo ni MKOPO FASTA wa Biashara na Mikopo ya Watumishi wa Umma katika mkutano na wanahabari uliyofanyika makao makuu ya benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Letshego Tanzania - Omar Msangi (katikati) akizungumza katika mkutano na wanahabari uliyofanyika makao makuu ya benki hiyo. Kulia ni Leah Phill - Meneja Mikopo ya Biashara na Denis Simon-Meneja wa Mikopo ya Watumishi wa Umma (kushoto).
Akizungumza katika uzinduzi huo mbele ya wanahabari Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Letshego Tanzania, Omar Msangi alisema;
“Mikopo hiyo ambayo ni hitaji kubwa kwa wafanyabiashara na Watumishi wa Umma wa Tanzania ni Mikopo rafiki inatolewa muda mfupi ili kuwawezesha wafanyabiashara na watumishi wa umma kutatua changamoto na kufanya maboresho ya shughuli zao kwa kadri ya mahitaji yao”.
Akizungumzia juu ya manufaa ya mikopo hiyo, Omar Msangi alisema, “itawaongezea wateja tija na uwezo wa kuboresha biashara na maisha yao na pia kutatua changamoto zao pasipo kuwa na wasiwasi wa kutokuwa na fedha za kutosha katika Biashara na shughuli zao za Kimaendeleo”.
Pia aliongeze kwa kusema, “MKOPO FASTA wa biashara utatolewa ndani ya saa 72 baada ya mteja kukamilisha fomu yake ya maombi wakati Mikopo ya wafanyakazi itatolewa ndani ya saa 48 baada ya mteja kukamilisha fomu yake ya maombi hivyo kumuwezesha mteja kutimiza malengo yake kwa wakati”.
MKOPO FASTA ni maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa, ambapo, ndani ya masaa 72, mfanyabiashara atapata mkopo wa hadi shilingi milioni 50, huku muda wa kurudisha mkopo ukifika hadi miezi 12.
Kwa upande mwingine, Mikopo ya watumishi wa umma inatolewa ndani ya saa 48 ambapo mwajiriwa wa serikali au taasisi ya umma anaweza kukopa hadi shilingi milioni 60 atakazozirejesha taratibu kwa hadi miezi 84.
Bi. Leah Phili, Meneja wa Mikopo ya Biashara alisema, “Mkopo Fasta kwa wafanyabiashara utawasaidia wafanyabiashara kuimarisha na kuboresha biashara zao. Ili tuweze kuboresha maisha kama dhima yetu inavyosema, tumejipanga kuhahikisha wateja wetu wanapata hela ndani saa 72 baada ya kukamilisha nyaraka muhimu za maombi ya MKOPO FASTA. Tunawakaribisha wafanyabiashara wote kutembelea matawi yetu au kutupigia simu kwa maelezo zaidi kuhusu huduma hii na pia kufanya maombi ya MKOPO FASTA.
Pia,Denis Simon ambaye ni Meneja wa Mikopo ya watumishi wa umma alisema, mikopo ya watumishi wa Umma inatolewa ndani ya Masaa 48 baada ya mteja kukamilisha tararibu zote za maombi ikiwepo kujaza fomu ya maombi na kuirudisha kwa afisa wa benki au tawi lolote lililo karibu nae.
Benki ya Letshego imefungua mlango kwa watumishi wote wa umma kupaya huduma rafiki za mikopo. Hali kadhalika, MKOPO FASTA ni huduma mahususi kwa mfanyabiashara yeyote aneohitaji fedha kwa haraka. Fomu za maombi zinapatikana katika matawi yote ya Benki ya Letshego na vituo vya kutolea huduma.
Kuhusu Benki ya Letshego Tanzania.
Benki ya Letshego ni Benki ya Biashara ambayo zamani ilijulikana kwa jina la Advans Bank ambayo ilianzishwa tangu Mwaka 2011. Ilipofika Mwezi in November 2015, Letshego Holding Limited walifanikiwa kupata 75% ya hisa za benki ya Advans Tanzania na hivyo kuanza rasmi kujulikana kwa jina la Letshego Bank (T) LTD mnamo August 2016. Mpaka sasa benki inamilikiwa kwa 100% na Letshego Holding Limited.
Benki ya Letshego Tanzania inatoa huduma mbalimbali kwa wateja wakubwa, wakati na wadogo kupitia matawi 5 (Dar es salaam 3, Mwanza na Mbeya), Vituo vya kutolea huduma 3 (Arusha, Tanga na Dodoma) Mashine za kutolea fedha zote za Umoja Switch na VISA, na Mawakala wa LetsGo Wakala zaidi 100.
Benki ya Letshego Tanzania Pia hutoa huduma kupitia simu za mikononi LetsGo Mobile kwa Mfumo wa USSD pamoja na App.