NA GODFREY NNKO
KAMATI ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imesema kuwa,mwenendo wa uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kutoka kwenye janga la UVIKO-19, ambapo ukwasi umeendelea kuwa wa kuridhisha na riba katika soko la mabenki kubakia katika viwango vya chini.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa leo Juni 6, 2022 na Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Gavana wa benki hiyo,Profesa Florens Luoga.
"Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania ilikutana Juni 6, 2022 kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi wa Tanzania na dunia katika kipindi cha Machi na Aprili 2022.
"Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha na matokeo yake, ambapo ukwasi uliendelea kuwa wa kuridhisha na riba katika soko la mabenki kubakia katika viwango vya chini. Hali hiyo iliendelea kuweka mazingira wezeshi kwa mabenki kutoa mikopo kwa sekta binafsi na riba nafuu,"amefafanua Prof.Luoga kupitia taarifa hiyo.
Pia kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati iliona kuwa tangu mkutano wake wa mwisho uliofanyika mwezi Machi 2022, uchumi wa dunia umeendelea kukabiliwa na changamoto ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei, bei za bidhaa, kuibuka upya kwa janga la UVIKO-19.
"Hivyo kuvurugika kwa mnyororo wa ugavi wa bidhaa na huduma kutokana na vita nchini Ukraine na vikwazo dhidi ya Urusi. Changamoto hizi zinaashiria kuongezeka kwa athari katika shughuli za kiuchumi,"ameeleza.
Aidha, kwa mujibu wa kamati hiyo, kwa upande wa Tanzania Bara, uchumi ulikuwa kwa asilimia 4.9 mwaka 2021, ikilinganishwa na lengo la asilimia 5 na kwa upande wa Zanzibar ukuaji ulikuwa asilimia 5.1, ikilinganishwa na lengo la asilimia 5.2.
Kamati imefafanua kuwa, mfumuko wa bei uliongezeka katika mwaka 2021/22 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia,kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa, hususan bei ya mafuta na bidhaa za walaji katika soko la dunia.
"Ujazi wa fedha uliongezeka kuendana na lengo, kutokana na utekelezaji wa sera ya fedha na kuimarika kwa mazingira na shughuli za kibiashara na uwekezaji. Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi umeendelea kuimarika kufikia asilimia 13.4.
"Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2022, mwenendo wa utekelezaji wa sera ya bajeti ni wa kuridhisha, ambapo mapato ya Serikali yameendelea kuimarika kutokana na ongezeko la shughuli za uchumi na ulipaji kodi.
"Sekta ya nje ilikabiliwa na changamoto zitokanazo na vita nchini Ukraine, ongezeko la bei za bidhaa na kuwepo kwa UVIKO-19,"amefafanua Prof.Luoga.
Hata hivyo, amefafanua kuwa akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha kufikia takriban dola za Marekani bilioni 5.5 mwezi Aprili 2022, na hivyo kuendelea kusaidia uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi.
Prof.Luoga amefafanua kuwa, thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni imeendelea kuwa tulivu mwaka hadi mwaka, ambapo ilipungua dhidi ya dola ya Marekani kwa kiwango cha chini ya asilimia moja.
Amesema, Kamati ya Sera ya Fedha ilipokea taarifa kuhusu kupitishwa kwa Kanuni za Fedha za Kigeni, 2022, mwezi Mei, ambazo zinaruhusu wakazi wa nchi za SADC, pamoja na wakazi wa nchi za EAC, kushiriki katika kuwekeza kwenye dhamana za serikali, na wakazi wa Tanzania kuwekeza katika nchi hizo.
"Ushiriki wa wakazi wa nchi hizo utaongeza wigo wa wawekezaji na ushindani katika soko la dhamana za Serikali.
Kwa kuzingatia tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania na dunia, Kamati ya Sera ya Fedha imeridhia Benki Kuu kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi kwa mwezi Mei na Juni 2022, ili kuendelea kuimarisha biashara na uwekezaji nchini.
Benki Kuu inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa shughuli za uchumi na ongezeko la mfumuko wa bei, ongezeko la bei za bidhaa, na athari za vita nchini Ukraine. Hatua zitachukuliwa kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo, ikiwemo kuanza kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi,"amefafanua Gavana wa Benki Kuu na Mwenyekiti wa kamati hiyo.