NA HUGHES DUGILO
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa wito kwa wafanyabiashara kote nchini kurasimisha biashara zao ikiwemo kufanya usajili ili kufanya shughuli zao kutambulika kisheria.
Wito huo umetolewa leo Juni 20,2022 na Ofisa Habari wa wakala huo, Bi. Christina Njovu katika soko Jipya la Mbagala Zakheim lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam walipokuwa wakifanya usafi ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza rasmi Juni 16 na yanatarajia kufikia tamati Juni 23, mwaka huu.
Njovu ameeleza kuwa, licha ya BRELA kufanya usafi sokoni hapo pia inawapa fursa wafanyabiashara hao kupata elimu juu ya kazi mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo ikiwemo usajili wa biashara na leseni.
"Leo tumefika hapa kufanya usafi katika soko hili, huu ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza wiki iliyopita hivyo BRELA tumekuwa tukifanya kazi mbalimbali za kijamii na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kazi zetu.
"Hii ni fursa kwa wafanyabiashara wa soko hili la Zakheim kuifahamu BRELA na kazi zake ili sasa wapate kurasimisha kazi zao kwa kusajili biashara zao,"amesema Njovu.
Ameongeza katika,Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma BRELA imeendelea kutoa huduma zake za papo kwa hapo katika viwanja vya ofisi zake zilizopo katika makutano ya mtaa wa Shaaban Robert na barabara ya Sokoine jijini Dar es Salaam na kwamba zoezi hilo litakamilika Juni 23,mwaka 2022.