NA DIRAMAKINI
TIMU ya Buswelu Veterans kutoka wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza wako katika hatua za mwisho za maandalizi ya safari kwenda kushindana na Veterans wenzao wa Mikoa ya Simiyu na Shinyanga.
Ziara hiyo itakayochukua siku nne itatoa fursa kwa timu ya Buswelu Veterans kucheza mechi tatu, ikianza tarehe 24 Juni mwaka na kukamilika tarehe 26, na timu kurejea Mwanza.
Akizungumzia safari hiyo, Mwenyekiti wa Buswelu Veterans, Sosthenes Bulugu amesema wameamua kufanya ziara hiyo ikiwa na lengo la ujirani mwema pamoja na kuongeza umoja, ushirikiano wa timu za Veterans Kanda ya Ziwa.
"Tumekuwa na utaratibu wa safari kama hizi na zimekuwa zinatusaidia kuleta ushirikiano na wenzetu ambao tunacheza mechi. Hii ni ishara ya kuongeza marafiki sambamba na kuzungumzia hali ya maendeleo ya soka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,"alisema Sosthenes Bulugu.
Kwa upande wake Katibu wa timu hiyo Alex Simon amesema kuwa, maandalizi kuelekea kwa safari hiyo yamekwisha kufanya ikiwa ni pamoja na wachezaji kujifua kwa mazoezi kabambe ili kujiweka imara kushindana na timu za Veterans kutoka Simiyu na Shinyanga.
Nahodha wa timu hiyo Juma Kisuse pamoja na Mchezaji mwandamizi Simon Romli wameupongeza uongozi wa Buswelu Veterans kwa kuwa na mikakati mizuri ya kuandaa safari ili timu ikashindane ugenini.
Kwa upande wake msemaji wa timu hiyo, Peter Onyango amesema msafara wa wachezaji na viongozi ishirini na sita utaondoka tarehe 24 Juni 2022 kueleka Busega Simiyu na kucheza mechi moja huko kabla ya kesho yake jumamosi kucheza mechi mjini Shinyanga na Jumapili kumalizia Kahama na kurejea Mwanza.