NA GODFREY NNKO
CHAMA cha Wasioona Tanzania (TLB) Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam kimeishukuru Nyumba Saccos Ltd kwa kuguswa na mahitaji yao, hivyo kuwawezesha kiasi cha fedha na fimbo za kutembelea.

Katibu wa chama hicho, Wilaya ya Temeke, Bw.Protase Mutakyanga amesema, Nyumba Saccos Ltd imewapa heshima ya kipekee kupitia msaada wao ambao wameupokea zikiwemo fedha taslimu na fimbo nyeupe.
"Tunawashukuru sana Nyumba Saccos kwa kutupatia fedha kiasi kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kiofisi zikiwemo fimbo 30. Ni jambo la heshima sana, kwa sababu tuliwaomba Nyumba Saccos fimbo chache,wao wakatuongezea zaidi, kwa kweli tunashukuru sana.
"Huu msaada utatusaidia kwa kiasi kikubwa kutatua baadhi ya changamoto ambazo zinatukabili,pia tunatoa wito kwa wadau wengine ndani ya Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam kuangalia namna ya kujumuika nasi katika masuala mbalimbali yanayotuhusu, sasa tumepata fimbo 30, lakini tuna upungufu wa fimbo 178, hivyo mchango wa wadau ni muhimu sana,"amesema.


Amesema, Nyumba Saccos licha ya kununua fimbo 30 na kuweka kiasi kidogo cha fedha katika akaunti ya chama hicho, wanaamini kadri njia na fursa zitakavyofunguka nao wataendelea kuyashika mkono makundi mbalimbali mkono kikiwemo chama hicho.
Pia amesema,wamezisikia na kuzipokea changamoto zinazowakabili wanachama wa chama hicho wilayani Temeke, hivyo watazifikisha katika ngazi husika ili pale ambapo kuna uwezekano wa wao kama chama au kwa kushirikiana na wadau wengine waweze kuzipatia ufumbuzi.

"Tumelipokea hilo kama chama na kwa sehemu tunaweza kulifikisha kwa wenzetu ili na wao ambao hawajawahi kuona kwamba kuna sehemu fulani kuna chama cha wasioona, tunapaswa na sisi tupeleke kitu fulani ili waweze kuwafikia na ninyi,"amesema Meneja wa Nyumba Saccos.
Pia Bi.Amini ametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum katika jamii wakiwemo wanachama wa chama hicho ili waweze kuyafikia malengo na ndoto zao.
Amesema, kufanya hivyo, si tu kunawawezesha kuyafikia malengo yao bali kunawapa moyo kuwa, mara zote jamii ya Watanzania ipo pamoja nao katika hali yoyote na mazingira wanayopitia.