NA ANGELA MSIMBIRA,OR-TAMISEMI
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji ya Maendeleo (UN Capital Development Fund-UNCDF) wanatarajia kutekeleza miradi yenye gharama ya shilingi milioni 343.9 kwa ajili kujenga uhimili wa athari za mabadiliko ya tabianchi (Local Climate Adaptive Living Facility - LoCAL).
Akifungua kikao kazi cha watekelezaji wa programU hiyo Juni, 2022 jijini Dodoma. Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. John Cheyo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia TAMISEMI, Bw. Ramadhan Kailima amesema programu hiyo ina lengo la kuwawezesha wananchi kujenga uhimili wa athari za mabadiliko ya tabianchi.
Bw. Cheyo amesema, programu inatekelezwa katika halmashauri tatu za Wilaya ya Chamwino, Mpwapwa na Kondoa zikiwa ni sehemu ya Halmashauri za kuanzia utekelezaji wa Mradi (Pilot Districts) ambapo fedha hizo zitatumika kuwawezesha wananchi kukabiliana na athari za mabadilko ya tabianchi hususan ujenzi wa miundombinu ya mifumo ya usambazaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya jamii majumbani na umwagiliaji.
Aidha, ameziagiza halmashauri zinazoanza kutekeleza programu hiyo kuhakikisha wanatoa matokeo bora ili kuinusuru jamii na kujenga imani kwa wafadhili kwa kuwa kwa kufanya hivyo,kutatoa fursa kwa wadau wengine kujitokeza kwa lengo la utekelezaji wa mradi huo nchi nzima
Wakati Huo huo mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Maendeleo (UNCDF), Bi. Aine Mushi amezitaka halmashauri zitakazotekeleza mradi huo kuhakikisha zinafanyakazi kwa uadilifu, utendaji kazi uliotukuka na kujituma ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya Tabia nchi nchini.
Aidha, amendelea kufafanua kuwa programu hiyo ina lengo la kuwawezesha wananchi kujenga uhimili wa athari za mabadiliko ya tabianchi na kujiletea maendeleo yao kwa kuwezesha fedha kutoka katika vyanzo vya kitaifa na kimataifa kufika katika ngazi za chini kabisa kama inavyoelekezwa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu – (SDGs), Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa Mwaka 2021 – 2026.