NA DIRAMAKINI
CHAMA cha Walimu (CWT) Mkoa wa Pwani Kitengo cha Wanawake kimeiomba jamii kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria pale wanapoona kuna viashiria vya ukatili wa kijinsia.
Katibu wa Chama cha Walimu Mkoa wa Pwani,Mwajuma Masenga amesema endapo taarifa hizo zitakuwa zikitolewa mapema zitaleta matokeo chanya katika vita ya kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wahusika kudhibitiwa mapema.
Ameyasema hayo juzi wilayani Kibaha mkoani Pwani kwenye mkutano uliofanyika ukiwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowakabili walimu wanawake wakiwa kazini.
Mwajuma amesema wanalaani vitendo hivyo ambavyo kwa sasa vinaripotiwa katika maeneo mbalimbali, lakini pia wanaiasa jamii kuungana kupiga vita vitendo hivyo visiendelee kutokea.
"Hata kwenye maeneo ya kazi tunatakiwa tuzungumze na watoto wasijenge mazoea ya kupokea zawadi kwa kila mtu hii pia itapunguza vitendo wanavyofanyiwa watoto wetu ambavyo baadhi yao wanaathirika kiafya na wengine kupoteza maisha,"anasema.
Naye Katibu wa Wanawake CWT mkoa wa Pwani, Mwalimu Mariam Mpunga amesema dhumuni lao ni kuhakikisha walimu wanawake wanafanyakazi kwa uadilifu ili kufikia malengo waliyojiwekea ikiwemo kutetea haki zao.
Mpunga aliendelea kusema walimu wanawake wanao wajibu wa kutetea haki zao wenyewe,lakini pia kuhakikisha wapambana kwa hali na mali ili kuwalinda wanawake na watoto shuleni na majumbani.
Kwa upande wake mjumbe kamati tendaji CWT Taifa, Herbet Ngimi na Shabani Tesua walisema walimu pia wanatakiwa kujenga urafiki na wanafunzi na wanapobaini shida watafute namna ya kukabiliana nayo kwa kuwashirikisha wazazi.
Katika mkutano huo Mweka Hazina wa CWT Taifa,Aboubakar Alawi aliwataka walimu kujenga ushirikiano na kuepuka migogoro kazini.