Elimu ya madhara vitendo vya ukatili yazifikia shule 48 wilayani Serengeti

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu lenye makao Makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii, Dawati la Jinsia na Watoto (Polisi) na Ustawi wa Jamii wameweza kutoa elimu ya madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika shule 48 za msingi wilayani Serengeti na kuunda klabu za wanafunzi wa kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia.
Utoaji wa elimu hiyo umeenda sambaba na kuadhimisha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo kila mwaka kilele chake hufanyika Juni 16, hivyo wanafunzi hao wameelimishwa juu ya haki zao na wajibu wao katika kujenga taifa imara na kizazi cheye tija. 

Huku jamii ikihimizwa kuwasaidia watoto wa kike kuwapa mahitaji yao ikiwemo taulo za kike na kuwawekea mazingira wezeshi wafike mbali zaidi kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla. 
Elimu hiyo, ililenga kuwafanya wanafunzi hao wawe na ufahamu wa kujua madhara ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, na aina nyingine za ukatili na jinsi ya kuchukua tahadhari hususani msimu huu wa ukeketaji wilayani humo kutokana na mwaka huu kugawika kwa mbili. 
Pia elimu hiyo ilikuwa ni kuwajenga wanafunzi hao wawe mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na wajue wapi sehemu sahihi ya kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vya ukatili vikitaka kufanyika ili kuweza kuvidhibiti ambapo wamehimizwa kutoa taarifa kwa Walimu wao, Polisi, Dawati la Jinsia na watoto pamoja na kwa watu wa kuaminika. 

Afisa Mwelimishaji Jamii Madhara ya Vitendo vya ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la Hope for Girls Women in Tanzania,Emmanuely Goodluck amesema,kupitia elimu hiyo ambayo wameitoa kwa pamoja na serikali wanafunzi wemefundishwa madhara ya Ukatili wa Kijinsia ikiwemo ukeketaji, haki za binadamu na jinsi ya kupinga mila potofu zinazowafanya wasitimize ndoto zao.
"Tumetoa elimu hii kwa pamoja na tumeunda klabu za wanafunzi kila shule kusudi mwamko na ushiriki wa kupinga vitendo vya ukatili uweze kufanikiwa. Nawashukuru Dawati la Jinsia na Watoto, ustawi wa Jamii, maendeleo ya jamii tumefanya kazi hii kwa pamoja ya kuelimisha na kuweka mikakati thabiti hasa msimu huu wa ukeketaji ambapo koo nyingi zimejipanga kukeketa. Ninaamini kwamba ushiriki wa kila mmoja utawezesha mabinti wasifanyiwe vitendo hivyo na pia hatua kali za kisheria zitachukukiwa dhidi ya wote watakaobainika,"amesema Goodluck.

Aidha, Goodluck amewashauri Wazee wa Kimila kuwa sehemu ya kukomesha vitendo vya ukeketaji katika Jamii kwani wananafasi hiyo kutokana na kuaminika na ushawishi wao. Huku jamii akiihimiza kuwafichua wote wanaofanya ukatili ili kujipatia kipato ili hali wanadidimiza ndoto za Watoto wa kike ambao ni Muhimu kwa maendeleo ya jamii na Taifa, hivyo kila mmoja awe mlinzi wafikie ndoto zao. 
Amesema, Shirika hilo kupitia Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly litaendelea kutoa elimu ya Ukatili wa Kijinsia kwa jamii kwa njia ya mikutano ya hadhara, makongamano, na njia mbalimbali sambamba na kushirikiana na serikali kwa karibu kumaliza ukatili. Huku wasichana wanaokimbia ukatili na kukimbilia katika vituo vinavyomilikiwa na shirika hilo kikiwemo Kituo cha "Hope Mugumu Nyumba Salama" na "Nyumba Salama Butiama" wataendelezwa kielimu na katika fani kama ambavyo limekuwa likifanya kufikia ndoto zao. 
Paul Mathias na Jesca Marwa ni Wakazi wa Mugumu wakizungumza na DIRAMAKINI kuhusu maoni yao juu ya zoezi hilo la utoaji wa elimu wamesema litaimarisha ushiriki wa wanafunzi kupinga ukatili na kuwaelimisha wazazi na walezi wao.

"Elimu hii ninatumaini wataifikisha kwa wazazi na walezi wao na watatoa msukumo thabiti namna gani mzazi aone mila ya ukeketaji haina faida na pia kuozesha mtoto kabla hajamaliza masomo yake ni kufifisha ndoto zake si hivyo tu...bali pia ulinzi wa mtoto na uzingatiaji wa haki za binadamu ni Muhimu kwa Ustawi bora wa jaii yetu,"amesema Jesca Marwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news