Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akienda mbele ya wabunge kusoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 7 wa Bunge la 12, bungeni jijini Dodoma, Juni 30, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
UTANGULIZI
Shukurani
1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha kuhitimisha shughuli zote za Mkutano wa Saba wa Bunge la Kumi na Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tukiwa buheri wa afya.
2. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukushukuru wewe binafsi kwa kuongoza vema mijadala ya Mkutano huu wa Saba wa Bunge la Kumi na Mbili. Waheshimiwa Wabunge, mtakubaliana nami kwamba katika kipindi hiki kifupi tangu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Mbunge wa Mbeya Mjini ashike wadhifa wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonesha ukomavu, uhodari na umakini mkubwa katika kuliongoza Bunge hili tukufu.
3. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninawapongeza sana Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala na Naibu Spika wa Bunge la Kumi na Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Wenyeviti wa Bunge Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini na Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalumu kwa kuonesha umahiri na weledi mkubwa katika kumsaidia Mheshimiwa Spika kuhakikisha shughuli zote za mkutano huu zinakamilika kama zilivyopangwa.
4. Mheshimiwa Spika, kipekee, ninawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri kwa kuwasilisha kwa umahiri mkubwa hoja za bajeti za Wizara zao, kutoa ufafanuzi wa kina pamoja na kujibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mijadala ya hoja hizo. Ni matumaini yangu kwamba baada ya kuhitimishwa kwa shughuli za Mkutano huu, sasa watakwenda kusimamia ipasavyo sekta zao ili kuhakikisha bajeti zilizowasilishwa zinagusa maeneo ya msingi na maslahi mapana ya Watanzania.
5. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitotambua ushiriki mzuri na michango ya Waheshimiwa Wabunge wenzagu wakati wote wa Mkutano huu tangu ulipoanza tarehe 5 Aprili 2022. Ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwani michango na ushiriki wenu umekuwa chachu katika kufanikisha shughuli za Mkutano wa Saba wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan katika kutekeleza kikamilifu wajibu wetu wa Kikatiba wa kupitia, kujadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.
6. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii, kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali kwa upande wake itazingatia maoni na ushauri wao kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Watanzania.
Aidha, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuwa katika kipindi hiki tunaporejea majimboni kwetu tukawe mabalozi wazuri kwa wananchi tunaowatumikia kuhusu mambo mengi muhimu yaliyojiri katika kipindi chote cha Mkutano huu hususan mipango na mwelekeo wa Serikali katika kipindi cha mwaka 2022/2023.
Salamu za Pole
7. Mheshimiwa Spika, tarehe 24 Aprili 2022 wakati tukiendelea na shughuli za Mkutano wa Saba wa Bunge lako tukufu, tulipokea taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Irene Ndyamukama, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi kilichotokea katika Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha, mkoani Pwani. Hivyo basi, nami kwa masikitiko makubwa naungana tena na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa salamu za pole kwako Mheshimiwa Spika, kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu kufuatia kuondokewa na mpendwa wetu.
8. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, pia tumeshuhudia kutokea kwa ajali mbalimbali za vyombo vya usafiri zikihusisha pikipiki, magari, treni n.k. Ajali hizo, zimesababisha vifo vya wapendwa wetu, uharibifu wa mali na pengine ulemavu. Kwa msingi huo, nitoe pole kwa Watanzania wenzangu waliopoteza wapendwa wao na wengine kupata majeraha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matukio ya ajali za vyombo vya usafiri. Niwatakie afya njema na uponyaji wa haraka wale wote waliojeruhiwa na tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi. Amina.
SHUGHULI ZA BUNGE
9. Mheshimiwa Spika, sambamba na kupitia, kujadili na hatimaye kupitisha Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023, Bunge lako tukufu pia lilipata fursa ya kupokea maswali kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na kutolewa majibu kutoka upande wa Serikali. Shughuli nyingine zilizotekelezwa ni kujadili na kupitisha miswada ya sheria, maazimio ya Bunge na kupokea kauli za Serikali katika kutolea ufafanuzi hoja kadhaa zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge ambazo zilihitaji kupata kauli ya Serikali.
Maswali na Majibu
10. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Saba wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jumla ya maswali 487 ya msingi na mengine 2,622 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Halikadhalika, jumla ya maswali 27 ya papo kwa papo yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Miswada
11. Mheshimiwa Spika, jumla ya Miswada ya Sheria minne iliweza kujadiliwa na kupitishwa na Bunge lako tukufu. Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 wa Mwaka 2022 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji wa Mwaka 2022 ilisomwa kwa mara ya kwanza.
12. Mheshimiwa Spika, vilevile, Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2022 na Muswada wa Sheria wa Kuidhinisha Matumizi ya Serikali ilisomwa kwa hatua zake zote.
Maazimio
13. Mheshimiwa Spika, vilevile, Bunge lako tukufu lilifanikiwa kujadili na kupitisha Maazimio matatu ya Bunge yafuatayo: -
Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa duniani na kupewa tuzo ya juu ya Mjenzi Mahiri ya Babacar Ndiaye kufuatia mafanikio makubwa katika ujenzi wa miundombinu;
Azimio la Bunge la kuipongeza timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu (Serengeti Girls) baada ya kufuzu michuano ya kombe la dunia itakayofanyika nchini India; na
Azimio la Bunge la kuipongeza timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wenye Ulemavu (Tembo Warriors) kufuatia kufuzu michuano ya kombe la dunia itakayofanyika nchini Uturuki.
Kauli za Serikali
14. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia Kanuni ya 56 ya Kanuni za Kudumu za Bunge za Mwaka 2020, Waheshimiwa Mawaziri walitoa kauli rasmi za Serikali Bungeni ikiwa ni ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. Hoja hizo, zilihusu baadhi ya mambo yaliyotokea nchini na kugusa moja kwa moja maslahi ya wananchi. Kauli zilizotolewa ni kama ifuatavyo: -
(i) Wizara ya Nishati
15. Mheshimiwa Spika, kupitia Mkutano huu Mheshimiwa Januari Yusuf Makamba (Mb.), Waziri wa Nishati alitoa Kauli ya Serikali Bungeni kuhusu kupanda kwa bei za mafuta na hatua zinazochukuliwa kushughulikia suala hilo. Serikali pamoja na mambo mengine ilitoa mwenendo wa bei ya mafuta, mipango ya muda mfupi na mrefu ya kukabiliana na changamoto hiyo pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa ikiwemo kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 ili kupunguza makali ya bei ya mafuta nchini.
(ii) Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
16. Mheshimiwa Spika, vilevile, Mheshimiwa Hamad Masauni (Mb.), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alitoa Kauli ya Serikali Bungeni kuhusu Watanzania waliopo Nje ya Nchi kurudi nchini kushiriki shughuli za Ujenzi wa Taifa. Kauli hiyo, imezingatia hali nzuri ya kisiasa na kiusalama nchini pamoja na hatua za dhati zinazochukuliwa na Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kila mtanzania wakiwemo viongozi wa kisiasa waliopo ndani na nje ya nchi wanashiriki katika shughuli za ujenzi wa nchi yao.
MWELEKEO WA SERIKALI YA AWAMU YA SITA
17. Mheshimiwa Spika, leo tunaelekea kuhitimisha shughuli za Mkutano wa 7 wa Bunge la Kumi na Mbili. Aidha, kupitia Mkutano huu, pamoja na mambo mengine Bunge lako tukufu limefanikiwa kupitia, kujadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023. Bajeti tulioipitisha imeendelea kututhibitishia nia njema, uthubutu wa hali ya juu na azma ya kweli ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutelekeza mipango na mikakati mbalimbali yenye lengo la kuwaletea watanzania maendeleo ya haraka sambamba na kuwakwamua kiuchumi.
18. Mheshimiwa Spika, mengi yameelezwa na kufafanuliwa na Waheshimiwa Mawaziri wakati wakiwasilisha hoja za bajeti za sekta zao, na wakati mwingine hata Waheshimiwa Wabunge wakati walipokuwa wakichangia hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Serikali kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri. Kwa lugha nyingine, kupitia hotuba hii ya kuhitimisha shughuli za Serikali zilizopangwa kwenye Mkutano wa 7 wa Bunge la 12, nisingependa kurudia kile kilichokwisha jadiliwa wakati wote wa Mkutano huu.
19. Mheshimiwa Spika, hata hivyo, niruhusu nitumie fursa hii kugusia kwa uchache baadhi ya mambo ya msingi ambayo yanaakisi taswira, dhamira, nia, uthubutu, maono na azma ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha taifa letu linapiga hatua za haraka za maendeleo ndani ya kipindi kifupi. Miongoni mwa mambo hayo ni ujio wa Filamu ya Royal Tour; ujenzi wa miradi ya maji katika miji 28 na kuwekwa saini kwa Makubaliano ya Awali ya Utekelezaji wa Mradi wa Usindikaji Gesi Asilia (LNG).
Filamu ya Royal Tour
20. Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu litakubaliana nami kwamba sekta ya utalii imeendelea kupata mafanikio makubwa hususan kufuatia uzinduzi wa filamu ya Royal Tour tarehe 28 Aprili, 2022 Jijini Arusha. Filamu hiyo ya kihistoria imekuja katika kipindi muhimu ambacho sekta ya utalii na huduma ilikumbwa na athari za UVIKO-19. Hivyo, ujio wa filamu hiyo, umechangia kuimarisha shughuli za utalii na kusaidia kwa kiwango kikubwa kuondoa sintofahamu nyingi kuhusu urithi wa utalii uliopo Tanzania. Mheshimiwa Rais ameweza kuonesha uhalisia wa nchi yetu kuanzia vivutio vya biashara, utalii, madini na hata sanaa na utamaduni wetu.
21. Mheshimiwa Spika, matunda ya jitihada hizo za Mheshimiwa Rais yameanza kuonekana hususan kwenye sekta ya utalii na huduma ambapo watalii na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani wameanza kumiminika nchini. Mathalan, watu maarufu wakiwemo wachezaji wa mpira wa miguu kutoka ligi kuu mashuhuri barani ulaya na ligi ya mpira wa kikapu nchini Marekani wametembelea Tanzania katika kipindi hicho. Kadhalika, wakala wa utalii zaidi ya 30 kutoka katika masoko ya utalii yakiwemo Marekani, Israeli, Ufaransa na Lithuania wamehamasika kuja nchini ili kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa lengo la kuvitangaza katika nchi zao.
22. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, mwezi Aprili, 2022 Serikali iliingia makubaliano na Jiji la Dallas lililopo nchini Marekani kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya utalii, biashara na uwekezaji. Hatua hiyo, inalenga kufungua fursa za usafiri wa anga kwa kuwezesha safari za moja kwa moja za ndege kutoka Tanzania hadi Dallas, Marekani.
23. Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ya utalii nchini ili kufikia lengo la kuvutia watalii milioni 5 kwa mwaka sambamba na mapato ya Dola za Marekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025. Kuongezeka kwa idadi ya wageni wanaotembelea Tanzania, kutaimarisha sekta ya utalii na huduma nchini na hivyo, kutengeneza fursa nyingi zaidi za ajira, kuwakwamua wananchi kiuchumi na kujenga uchumi imara na shindani.
Ujenzi wa Miradi ya Maji katika Miji 28
24. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa tangu akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa alijipambanua na mpango maarufu wa kumtua ndoo mama kichwani. Dhamira hiyo ya Mheshimiwa Rais imeendelea kujidhihirisha kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miradi ya maji katika miji 28 uliozinduliwa tarehe 6 Juni, 2022.
25. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 utachangia kwa kiwango kikubwa katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye miji iliyobainishwa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mradi huo wa maji ambao ni mkubwa zaidi kuwahi kutekelezwa nchini kwa wakati mmoja, utakapokamilika utahakikisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi wapatao milioni sita.
26. Mheshimiwa Spika, sambamba na upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira, miradi hiyo pia itakuwa chachu kwenye kuvutia uwekezaji hususan wa viwanda. Serikali kwa upande wake, itahakikisha kuwa ujenzi wa miradi ya maji kwenye miji 28 unafungua fursa nyingine za kiuchumi zikiwemo ajira kwa wananchi wetu hasa kwenye maeneo ambayo miradi hiyo itatekelezwa. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuwasihi watanzania wenzangu kuchangamkia fursa zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo ili kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi.
27. Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, niwasihi viongozi na Waheshimiwa Wabunge wenzangu tushirikiane katika kuimarisha usimamizi wa miradi hii pamoja na kuhakikisha wakandarasi wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati ili miradi hiyo iweze kutoa huduma iliyotarajiwa kwa wananchi. Vilevile, niwasihi Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa vinara katika kuhamasisha wananchi kutunza mazingira na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji kwani uhifadhi wa mazingira ndiyo msingi wa uendelevu wa upatikanaji wa majisafi na salama.
Utekelezaji wa Mradi wa Usindikaji Gesi Asilia (LNG)
28. Mheshimiwa Spika, sote tumekuwa miongoni mwa mashuhuda wa kusuasua kwa muda mrefu kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa uchakataji wa Gesi Asilia (LNG). Kwa msingi huo, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikiwa kutegua kile kitendawili cha muda mrefu cha lini ungeanza utekelezaji wa mradi wa uchakataji wa Gesi Asilia (LNG) uliosimama kwa muda mrefu.
29. Mheshimiwa Spika, kufuatia juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, tarehe 11 Juni, 2022 tulishuhudia kuingiwa kwa makubaliano ya awali ya Mkataba wa Nchi Hodhi na Kampuni za Kimataifa za Utafutaji Mafuta kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa LNG.
30. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha azma ya Mheshimiwa Rais inatimia nitumie fursa hii kutoa wito kwa viongozi na watendaji wa sekta husika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi wa LNG unaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa taifa letu ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya Serikali yatokanayo na mauzo ya gesi, kuzalisha ajira za muda mfupi na za kudumu na kuimarisha mapato na uchumi wa watanzania kupitia mauzo ya bidhaa na huduma mbalimbali wakati wa utekelezaji wa mradi.
31. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande wake itaendelea kuhakikisha kuwa inavutia uwekezaji unaokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 30 kutoka nje kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Vilevile, ninaielekeza Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa inatumia vema fursa ya uwepo wa mradi wa LNG kuimarisha uzoefu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) katika shughuli za gesi pamoja na kuwezesha upatikanaji wa gesi asilia iliyochakatwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
UJENZI WA MJI WA SERIKALI
32. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022, Mheshimiwa Rais aliridhia takriban shilingi bilioni 600 zitumike kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi wa majengo 25 ya wizara na taasisi kwenye Mji wa Serikali uliopo Mtumba jijini Dodoma. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba ujenzi huo unaendelea vizuri na hadi kufikia tarehe 24 Juni 2022 umefikia kati ya wastani wa asilimia 30 hadi asilimia 56.
33. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuzihimiza wizara na taasisi kuhakikisha wanaimarisha usimamizi ili ujenzi ukamilike ndani ya muda uliopangwa. Nitoe rai pia kwenu Waheshimiwa Wabunge mnapoondoka hapa Bungeni mpate muda kidogo wa kutembelea na kuona kazi nzuri inayoendelea kwenye mji huo.
UWAJIBIKAJI KATIKA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
34. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha dhamira nzuri ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa inayojiakisi kwenye Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 inafikiwa, Serikali imejipanga vema kuendelea kusimamia suala la uwajibikaji katika utumishi wa umma. Mikakati iliyopo katika kuimarisha uwajibikaji hususan kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni kama ifuatavyo: -
Moja: Kuongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka shilingi bilioni 57.44 hadi shilingi bilioni 79.09 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hizo. Sambamba na ongezeko hilo la Bajeti katika mwaka 2022/2023, Serikali pia, imehuisha muundo wa Sekretarieti za Mikoa kwa kuboresha iliyokuwa Sehemu ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa na kuwa Sehemu ya Menejimenti, Ufuatiliaji na Ukaguzi ili kuimarisha ufuatiliaji wa mapato, matumizi na utekelezaji wa miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa;
Mbili: Kuendelea kuwajengea uwezo Waheshimiwa Mameya, Wenyeviti wa Halmashauri na Miji, Madiwani, Mafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kupitia Programu ya Uimarishaji Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Lengo ni kuongeza uelewa wa majukumu yao kisheria, kuimarisha mahusiano yao na viongozi wa kisiasa na kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao pamoja na ukusanyaji wa mapato; na
Tatu: Kupima utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kutumia viashiria muhimu hususan usimamizi wa mapato na makusanyo ya ndani, upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo, usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ikiwa ni pamoja na marejesho, usimamizi wa miradi ya maendeleo na uzuiaji na utekelezaji wa hoja za ukaguzi zinazoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
MASUALA YA UFUATILIAJI NA TATHMINI
35. Mheshimiwa Spika, eneo jingine lenye lengo la kuimarisha utendaji na uwajibikaji Serikalini ni tasnia ya ufuatiliaji na tathmini. Tasnia hii mtambuka inahitaji uwepo wa mifumo na miundo imara ambayo itawezesha kujenga msingi thabiti wa usimamizi wa utendaji kazi wa Serikali. Kwa kuzingatia hilo, Serikali inaendelea kujenga mifumo na miundo wezeshi katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuboresha utendaji kazi unaojali matokeo.
36. Mheshimiwa Spika, hatua hizo zinajumuisha kupitia upya miundo na majukumu ya Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuziimarisha pamoja na kujenga uwezo wa watumishi katika eneo hilo.
37. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Serikali imeanza maandalizi ya Sera ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa kuzihusisha taasisi simamizi zinazohusika na ufuatiliaji na tathmini ili kuchambua maeneo wanayosimamia na kuhakikisha maeneo yote muhimu yanajumuishwa ikiwemo usimamizi wa mipango ya maendeleo na utendaji wa Serikali kwa ujumla.
38. Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo, tayari, Serikali imekamilisha Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo ambao utaanza kutumika Julai, 2022. Mfumo huo, pamoja na mambo mengine utasaidia Serikali kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hivyo kuongeza tija na thamani ya matumizi ya fedha za umma kwenye miradi husika.
39. Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imehuisha Muundo na Mgawanyo wa Majukumu wa Ofisi ya Waziri Mkuu hususan kwa upande wa Sera, Uratibu na Bunge ili kuimarisha jukumu la ufuatiliaji na tathmini. Lengo ni kuhakikisha taarifa za ufuatiliaji na tathmini kutoka katika wizara na taasisi za Serikali zinafanyiwa uchambuzi wa kina pamoja na kutoa mrejesho kuhusu utendaji wa Serikali.
40. Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Fedha na Mipango kufanyia kazi changamoto ya uhaba wa wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini; kazi za tathmini kufanyika kwa ufanisi na uwepo wa mifumo mingi ya ukusanyaji wa taarifa yenye kuathiri ubora wa takwimu.
41. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanya tathmini ya ujuzi unaohitajika, kufanya tathmini ya mifumo ya ufuatiliaji na tathmini iliyopo kwenye taasisi za Serikali, kuandaa Kanzi-Data ya watumishi wenye utaalamu wa masuala ya ufuatiliaji na tathmini, kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye ufuatiliaji na tathmini na kuimarisha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini ili kujenga mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini ambao utawezesha kufuatilia, kuchambua na kupata taarifa halisi na kwa wakati za utendaji wa Serikali.
ULINZI NA UHIFADHI WA MAZINGIRA
42. Mheshimiwa Spika, suala la kulinda na kuhifadhi mazingira limeendelea kuwa moja ya vipaumbele muhimu vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais katika hotuba zake mbalimbali ndani na nje ya nchi, amekuwa akisisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa ustawi wa jamii yetu na kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu.
43. Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu ambazo siyo endelevu na rafiki wa mazingira zikiwemo ukataji wa miti hovyo, uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu, ukataji wa miti holela kwa ajili ya uchomaji wa mkaa, uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na uchomaji moto misitu yetu zimekuwa zikichangia sana uharibifu wa mazingira nchini. Jitihada zinazofanywa na Serikali kuhifadhi mapori yetu ni katika kulinda tunu zilizopo kwenye maeneo muhimu kama vile Loliondo, Ngorongoro, Selou, Ruaha, Katavi n.k.
Pori Tengefu la Loliondo
44. Mheshimiwa Spika, Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,000 limekuwa likitumiwa na wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, ulishaji wa mifugo na makazi. Serikali kwa upande wake imeendelea kulitumia katika shughuli za uhifadhi na utalii. Aidha, matumizi yasiyo rafiki yamekuwa chanzo cha kuharibika kwa mfumo ikolojia wa Pori hilo.
45. Mheshimiwa Spika, Pori Tengefu Loliondo ni muhimu kwa ajili ya kulinda Mfumo Ikolojia ya Serengeti, ikiwemo maeneo ya mazalia, makazi na mapito ya makundi makubwa ya nyumbu wahamao. Sababu kubwa ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni kuhifadhi mzunguko wa nyumbu ambao kwa kiasi kikubwa uko upande wa Tanzania na umuhimu wake kama urithi wa dunia. Serikali imekuwa ikifanya mabadiliko pale ambapo imeonekana mzunguko huu uko hatarini na hivyo kuhakikisha kuwa unalindwa kikamilifu.
46. Mheshimiwa Spika, maeneo muhimu yanayohitaji kuhifadhiwa kwa lengo la kulinda mzunguko wa nyumbu ni maeneo ya mazalia na mapito kwenye eneo la kilomita za mraba 1,500 za Pori Tengefu la Pololeti. Maeneo mengine muhimu ni vyanzo vya maji ambavyo huingiza maji kwenye mito mikuu mitatu ya Nyabogati, Pololeti yenyewe na Grumeti.
47. Mheshimiwa Spika, uhifadhi wa maeneo haya ni muhimu ili kuinusuru ikolojia ya Serengeti ikiwemo Bonde la Seronera ambako mito hii humwaga maji yake na ndicho kitovu cha utalii ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. Kadhalika, eneo hilo la Pololeti - Loliondo linalopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, limeendelea kuwa eneo muhimu kwa ajili ya mtawanyiko wa wanyamapori hususan nyumbu, pundamilia na Pofu.
48. Mheshimiwa Spika, shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji na makazi zimekuwa chanzo cha uharibifu wa ikolojia niliyoielezea ambayo ni muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa hifadhi zetu hususan Serengeti. Vilevile, shughuli hizo zimechangia uharibifu wa uoto wa asili na kusababisha kukosekana kwa malisho na maji, kupungua uwezo wa kiuchumi kwa wafugaji. Aidha, ongezeko la mifugo limesababisha maeneo yote ya vyanzo vya maji na mito kuharibika. Uharibifu huo mkubwa wa mazingira, pia, umekuwa chanzo cha wanyamapori kutoweka.
49. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha uwepo wa matumizi endelevu ya Pori Tengefu la Loliondo, Serikali ilielekeza eneo la kilometa za mraba 1,500 lihifadhiwe na eneo lililobaki la kilometa za mrada 2,500 wananchi waendelee kulitumia kwa shughuli nyingine. Utekelezaji wa maelekezo hayo ya Serikali umehusisha zoezi la kuwekwa vigingi katika eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,500 la Pori Tengefu Pololeti - Loliondo.
50. Mheshimiwa Spika, zoezi hili la uwekaji wa vigingi ambalo limekamilika kwa asilimia 100 halitoathiri maendeleo ya wakazi wa eneo la vijiji 14 vinavyopakana na eneo hilo. Aidha, hakutakuwepo na Kijiji kitakachofutwa na hakuna miundombinu itakayoondolewa kwa kuwa ndani ya eneo la kilometa za mraba 1,500 la Pololeti hakuna miundombinu yoyote.
51. Mheshimiwa Spika, Serikali imesimamia kwa umakini mkubwa zoezi la uwekaji vigingi kwenye eneo la kilometa za mraba 1,500 ambalo ni muhimu kwa ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Halikadhalika, Serikali imeendelea kushirikiana na wananchi wa Loliondo katika kuboresha malisho ya mifugo, uchimbaji wa visima vya maji, ujenzi wa majosho pamoja na miundombinu ya kunyweshea mifugo kwenye eneo la kilometa za mraba 2,500.
52. Mheshimiwa Spika, pia, ninaielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa Sheria ya Ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 inatumika ipasavyo kutenga na kuweka mipaka ya vijiji. Serikali kwa kuzingatia matakwa ya wananchi hasa maeneo ya malisho kwenye vijiji 14 vilivyopo karibu na Pori Tengefu la Poloreti itaweka utaratibu utakaopangwa kwa pamoja baada ya kukamilisha zoezi la utambuzi wa mifugo kwenye vijiji husika kwa lengo la kuwezesha kuhudumia mifugo iliyopo ndani ya eneo hilo.
Hifadhi ya Ngorongoro
53. Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa matumizi mseto ya ardhi, takriban miaka 60 iliyopita, usimamizi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro umeshindwa kutimiza lengo la kuleta uwiano baina ya uhifadhi, ukuzaji wa utalii na maendeleo ya jamii kutokana na changamaoto mbalimbali. Hali hiyo imechangiwa na changamoto nyingi za kiuhifadhi na maendeleo ya jamii hususan ongezeko la idadi kubwa ya watu na mifugo, makazi holela na shughuli za binadamu. Kwa mfano, mwaka 1959 wakati Hifadhi hiyo inaanzishwa kulikuwa na watu takriban 8,000 na mifugo 161,000. Lakini hadi sasa idadi ya watu inakadiriwa kuwa takribani 110, 000 na mifugo zaidi ya 1,000,000. Ni jukumu la Serikali kuweka miongozo itakayowezesha maisha ya watu na uhifadhi kuwa endelevu kwa maslahi ya Taifa.
54. Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni kuendelea kudorora kwa ustawi wa maisha ya wenyeji wa Ngorongoro katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, uchumi, usalama wa chakula na lishe, ufinyu wa vyanzo mbadala vya mapato kwa jamii, makazi duni, kukosa haki ya msingi ya kikatiba ya kumiliki na kutumia ardhi kwa ajili ya maendeleo yao kwa sheria zilizopo, pia kumejitokeza kubadilika kwa uoto wa asili na kuenea kwa mimea vamizi. Hivyo, kuendelea kuwepo kwa mfumo uliopo, kunaathiri ustawi endelevu wa maliasili ambazo ndio chanzo kikubwa cha mapato ambayo hugharamia shughuli za maendeleo na ustawi wa Watanzania.
55. Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, Serikali kwa nyakati tofauti ilichukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto za usimamizi wa hifadhi ikiwemo kufanya tathmini ya kina tangu mwaka 2017 hadi mwaka 2021 kwa lengo la kutatua changamoto za mfumo wa matumizi mseto ya ardhi. Kutokana na tathmini hiyo, Serikali iliamua kutumia mapori Tengefu ya Handeni na Kitwai yaliyopo katika Wilaya za Simanjiro, Handeni na Kilindi kwa ajili ya wananchi wa Ngorongoro kuhamia na kuendeleza maisha yao na kujitafutia shughuli mbalimbali za uchumi.
56. Mheshimiwa Spika, sababu ya kutumia maeneo ya Handeni na Kitwai ni pamoja na kufaa kwa ufugaji na kilimo; mwingiliano wa kimila, kitamaduni na desturi katika ya jamii iliyopo Handeni na Kitwai na jamii ya wafugaji wa Ngorogoro na shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo zinafanana sana ambapo shughuli kuu ni ufugaji.
57. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha maeneo hayo yanakidhi makusudio yaliyotarajiwa, Serikali imeendelea kujenga miundombinu muhimu katika eneo la Msomera ikiwemo upangaji na upimaji wa viwanja vya makazi na mashamba na ujenzi wa nyumba 500 za wakazi ambapo ujenzi wa nyumba 103 umekamilika na ujenzi wa nyumba 400 unaendelea kupitia JKT. Vilevile, huduma za umeme na maji tayari zinapatikana na ujenzi wa shule ya msingi na sekondari umekamilika. Ujenzi wa miundombinu ya afya, majosho na barabara unaendelea.
58. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za eneo la Msomera lililopo Handeni kiuchumi na kijamii kupitia vikao vingi na wananchi wa eneo la Ngorongoro wakiwemo viongozi wa mila (Laigwanak), waheshimiwa madiwani, watendaji wa kata na vijiji (WEO na VEO) wawakilishi wa akinamama, vijana na wadau wengine. Hadi sasa, kumekuwa na mafanikio makubwa katika kusimamia utekelezaji wa zoezi hilo ambapo Serikali imeendelea kuhamasisha na kuandikisha zile kaya ambazo zipo tayari kuhama kwa hiari.
59. Mheshimiwa Spika, zoezi la kuandikisha wakazi wanaoomba kuhama kwa hiari linaendelea vizuri. Aidha, hadi kufikia tarehe 09 Juni 2022, jumla ya kaya 293 zenye watu 1,497 zilikuwa zimejiandikisha.
60. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wakazi wanaohama wanakuwa na maisha bora zaidi katika makazi mapya Msomera, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliridhia kutoa motisha mbalimbali kwa wakazi hao kama ifuatavyo:-
Moja: Kila Kaya inayoondoka inapewa fidia ya nyumba aliyokuwa anaishi;
Mbili: Kaya zote zinazohamia Msomera kwa hiari zinapatiwa nyumba zenye vyumba vitatu zilizojengwa kwenye eneo la ekari 2.5, godoro, tochi, na ndoo;
Tatu: Kila kaya inapewa shamba lenye ukubwa wa ekari tano na zitakabidhiwa hati za kumiliki ardhi kwa ajili ya eneo la nyumba na shamba. Pia lipo eneo lingine huru la kuchungia;
Nne: Kila kaya inapewa fedha za kutosha kwa ajili ya kuanzia maisha kwenye makazi mapya; na
Tano: Kila kaya inapewa mahindi magunia mawili kwa kipindi cha miezi mitatu kwa ajili ya kujikimu katika kipindi cha mpito wakati wakazi wakijiandaa na maandalizi ya kilimo.
61. Mheshimiwa Spika, upendo huo uliooneshwa na Mheshimiwa Samia, Rais wetu hauna budi kupongezwa na kila mwenye kuitakia mema nchi hii. Hata hivyo, utaratibu huu ni maalumu kwa Ngorongoro pekee. Leo tarehe 30 Juni, 2022 kaya nyingine 25 zenye jumla ya watu 115 zinatarajiwa kusafiri kwa hiari kuelekea Msomera na kuendelea na maisha yao kama kawaida. Nitumie nafsi hii kuwapongeza wananchi wote walioridhia kuhama kwa hiari. Tarehe 23 Juni 2022 nilitembelea Ngorongoro na nilipata fursa ya kuwaaga wananchi wanaohama kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera. Aidha, siku hiyo hiyo, nilitembelea eneo la Msomera lililopo Wilaya ya Handeni na kujionea wananchi waliohamia katika eneo hilo wakiendelea na shughuli zao kwa furaha ambapo waliishukuru sana Serikali na Mheshimiwa Rais kwa kuwaandalia makazi bora katika eneo hilo. Mheshimiwa Spika kwa ridhaa yako ninaomba tuwasikilize ..... (AUDIO CLIP).
62. Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa viongozi na watendaji kuendelea kuelimisha, kuhamasisha na kuwashirikisha wananchi na wadau wengine hususan wenyeji katika utekelezaji mzuri unaoendelea wa zoezi hilo.
Upandishwaji Hadhi wa Maeneo ya Mapori Tengefu kuwa Mapori ya Akiba
63. Mheshimiwa Spika, rasilimali za wanyamapori ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, hususan katika kukuza utalii na hivyo kuongeza pato la Taifa. Kwa msingi huo, mpango wa Serikali kupandisha hadhi baadhi ya mapori tengefu kuwa mapori ya akiba ni katika kuimarisha ulinzi wa rasilimali zilizopo katika mapori hayo kwa uhifadhi endelevu.
64. Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutangazwa kwa eneo lolote kuwa Pori la Akiba hufanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufuata taratibu zilizowekwa kisheria ikiwemo kufanya tathmini ya kina ya umuhimu wa eneo hilo katika uhifadhi na ushirikishwaji wa wananchi kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa za maeneo husika.
65. Mheshimiwa Spika, tathmini hiyo na ushirikishwaji wa wananchi husaidia Serikali kufanya maamuzi ya iwapo kuendelea na utaratibu wa kupandisha hadhi au la. Hivyo, naomba niwahakikishie wananchi wa maeneo husika ikiwemo Loliondo kwamba utaratibu wa kupandisha hadhi maeneo ya mapori hayo kuwa mapori ya akiba utasubiri mapitio ya pamoja kati ya Serikali na wananchi. Hivyo, Wizara isianze zoezi hilo hadi wananchi watoe maoni yao kwa maslahi ya pande zote.
KILIMO
66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka shilingi bilioni 294 katika mwaka 2021/2022 hadi shilingi bilioni 954. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 224 na limelenga kwenye maeneo yafuatayo: Utafiti wa kilimo, Uzalishaji wa mbegu, Umwagiliaji, Ujenzi wa maghala na Kuimarisha huduma za ugani.
67. Mheshimiwa Spika, malengo ya Serikali ni kuongeza ukuaji wa Sekta ya Kilimo kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 (Agenda 10/30); kuongeza mauzo nje ya nchi kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.2 hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 5 mwaka 2030; kupunguza umaskini kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka asilimia 28 kwas asa hadi chini ya asilimia 14 ifikapo 2025.
68. Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo hayo Serikali imepanga kuimarisha utafiti; kutoa ruzuku ya mbegu za alizeti, ngano na miche ya chikichi; kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo; kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo; kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo utakaowezesha upatikanaji wa pembejeo kwa mfumo wa ruzuku pindi inapotokea athari za kiuchumi na kuanza kutoa ruzuku ya mbolea mwaka 2022/2023.
69. Mheshimiwa Spika, ongezeko la bajeti kwa mwaka 2022/2023 linatarajiwa kuimarisha usalama wa chakula na lishe na hivyo kupunguza mfumuko wa bei ya chakula nchini; kuongeza eneo la umwagiliaji; kuongeza upatikanaji wa ajira kwa vijana na wanawake katika kilimo zitakazofikia milioni moja ifikapo mwaka 2025. Manufaa mengine ni kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwenye viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za kilimo kufikia asilimia 100 ifikapo 2030.
70. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na athari za kupanda kwa bei ya mbolea duniani, Serikali itaimarisha mfumo wa utoaji ruzuku ambapo tunatarajia kutumia Shilingi Bilioni 150 kutoa ruzuku ya mbolea kwa mazao yote. Kwa kipekee mfumo wa utoaji wa ruzuku utawalenga wazalishaji wa ndani. Aidha, kwa kipekee makampuni ambayo hayataungana na Serikali katika mfumo huu Serikali hatutosita kuwafutia leseni ya kuendesha biashara ya mboloea nchini.
MAELEKEZO MAHSUSI
71. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimekuwa na zinakusudia kuleta matokeo chanya na ya haraka kwenye nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Kwa msingi huo, nami ningependa kusisitiza na kuelekeza utekelezaji wa masuala yafuatayo: -
I: Kuimarisha matumizi ya TEHAMA na kuhakikisha mifumo ya TEHAMA inayotumiwa na mamlaka mbalimbali za Serikali inazungumza
72. Mheshimiwa Spika, Serikali imepata mafanikio mbalimbali katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA, ikiwemo kuunganisha taasisi zaidi ya 700 katika mfumo mmoja wa malipo GePG. Hivi sasa, Serikali inaweza kuona na kupata taarifa za makusanyo yote yaliyokusanywa kwenye taasisi zake kupitia mfumo uliounganishwa na mifumo mingine kama vile MUSE, GAMIS, TANePS, ERMS, HCMIS, LGRCIS, mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na mifumo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
73. Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio hayo makubwa Serikali imejenga mfumo maalum unaojulikana kama Government Enterprise Service Bus (GovESB) kwa ajili ya kuwezesha mifumo mbalimbali ya Mamlaka na Taasisi za Serikali kubadilishana taarifa na kuzungumza. Kwa msingi huo, ninaelekeza Wizara ya Fedha ishirikiane kwa karibu na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na wadau wengine muhimu kutekeleza yafuatayo: -
Moja: Kuhimiza taasisi za umma kuunganisha mifumo yao ya TEHAMA kupitia mfumo huu maalum;
Mbili: Kusimamia ujenzi wa mfumo wa Universal Billing System utakaotumiwa na taasisi ambazo hazina uwezo wa kujenga mifumo yao; na
Tatu: Kuhakikisha taasisi za umma zinajielekeza zaidi katika matumizi ya mifumo shirikishi pale ambapo taratibu za utendaji kazi zinafanana badala ya kila taasisi kujenga mfumo wake. Hakikisheni mifumo yote mipya ya TEHAMA inajengwa kwa kufuata Sheria, Taratibu, Kanuni, Viwango na miongozo inayosimamia matumizi ya TEHAMA katika utendaji wa Serikali.
II: Viongozi na Watendaji wa Serikali kuisemea na kutangaza mafanikio ya Serikali kwenye maeneo yao na sekta husika
74. Mheshimiwa Spika, baadhi ya wanazuoni wamewahi kusema kuwa uongo ukisemwa mara nyingi hugeuka kuwa ukweli. Nimeamua kurejea kauli hiyo kutokana na ukweli kwamba uzoefu wa mwaka mmoja wa uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaonesha kuwa yapo mafanikio lukuki tuliyoyapata kama nchi katika kipindi hicho. Hata hivyo, licha ya ukweli huo bado wananchi hawajaelezwa ipasavyo na wakati mwingine tumeacha upotoshaji kufanywa bila kusahihishwa au kuchelewa sana kusahihisha.
75. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa ni jukumu letu viongozi na watendaji wote kuhakikisha wananchi wanaelezwa kuhusu shughuli zinazofanywa na Serikali, mafanikio na changamoto zilizopo ninaelekeza viongozi na watendaji wote kuhakikisha wananchi wanapata haki yao ya kupata taarifa za Serikali kuhusu juhudi mbalimbali za kuwaletea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa mujibu wa ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
III: Mpango wa kutoa Elimumsingi Bila Ada
76. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake na dhamira njema ya kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 kuhusu Serikali kutoa Elimumsingi Bila Ada kwa ngazi ya shule za msingi na sekondari yenye kulenga kuimarisha mazingira ya utoaji wa elimu, mahudhurio na ufaulu.
77. Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji wa mpango huu, Waheshimiwa Wabunge wamelalamikia kuwepo utitiri wa michango shuleni. Aidha, Serikali kupitia waraka wa elimu na 5 wa mwaka 2015 na waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2015 imetoa maelekezo bayana kuhusu utekelezaji wa Elimumsingi Bila Ada ikiwemo matumizi ya fedha za utawala ambazo hutolewa HAZINA na kupelekwa moja kwa moja katika akaunti za shule za msingi na sekondari kwa ajili ya Vifaa vya kufundishia na kujifunzia, Ukarabati, Uendeshaji wa mitihani ya ndani na Utawala.
78. Mheshimiwa Spika, asilimia 10 ya fedha hiyo pia hutumika kugharamia huduma za umeme, maji na ulinzi. Hivyo basi, ninaagiza kuwa TAMISEMI kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote nchini kufuatilia matumizi na upatikanaji wa taarifa za matumizi ya fedha hizo pamoja na kuhakikisha hakuna michango holela inayotozwa kwa wanafunzi. Aidha, kuanzia sasa hakikisheni maelezo ya kujiunga na shule za umma (yaani Joining Instructions) yanahakikiwa na kupewa idhini na Katibu Tawala wa Mkoa husika kwa kushirikiana na Maafisa Elimu wa maeneo husika.
IV: Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022
79. Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ambalo ningependa kulitolea msisitizo ni utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. Kama mnavyofahamu, tarehe 23 Agosti 2022 imepangwa kuwa siku ya Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022. Zoezi hilo lilitanguliwa na Operesheni ya Anwani za Makazi ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 95 na Serikali imefanikiwa kukusanya taarifa na kutoa anwani za makazi zaidi ya milioni 12.
80. Mheshimiwa Spika, sambamba na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi ninaelekeza kama ifuatavyo: -
Moja: Taasisi zote zenye dhamana ya masuala ya ardhi na makazi kuhakikisha zinakuja na mikakati thabiti ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi iliyoainishwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi pamoja na kutoa miongozo ya namna bora ya kushughulikia changamoto za watanzania wenzetu kuishi katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria ili kuhakikisha wananchi wote wananufaika na fursa zitokanazo na zoezi hilo;
Mbili: Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha kuwa Mpango wa Uendelezaji wa Mfumo (System Sustainability Framework) unaotoa mwongozo wa shughuli zote za anwani za makazi zitakavyofanyika unatumika vizuri ili kufanya zoezi hili kuwa na thamani wakati wote;
Tatu: Viongozi katika ngazi zote hususan kwenye Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe kuwa jamii inaendelea kuelimishwa ili kujua manufaa sanjari na kulinda miundombinu ya anwani za makazi kwenye maeneo yao;
Nne: Wizara zote, Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa endeleeni kushughulikia changamoto zote zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi na kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu; na
Tano: Uhakiki wa majina ya mitaa katika vibao uendelee kufanyika ili kujiridhisha na usahihi wake na muonekano wake.
81. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 yanaendelea vizuri na yamefikia asilimia 87. Aidha, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu hususan mnaporejea kwenye maeneo yao ya uwakilishi kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye zoezi hilo muhimu. Vilevile, nitoe wito kwa watanzania wote kujiandaa kuhesabiwa ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Makarani wa Sensa na viongozi wetu kwenye maeneo tunayoishi.
MICHEZO
82. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa michezo nitumie fursa hii kuipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kupaisha mchezo wa soka nchini na kuifanya ligi ya Tanzania kuwa kivutio kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
83. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninaipongeza Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 17 maarufu Serengeti Girls kwa kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Oktoba mwaka huu nchini India. Tunawatakia kila la heri wawakilishi wetu hao ambao wataungana na Morocco na Nigeria kuiwakilisha Afrika na kukamilisha idadi ya timu 16 zitakazoshiriki fainali hizo za Dunia zikiwa ni fainali za saba tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 2008.
84. Mheshimiwa Spika, naipongeza pia Timu ya Taifa ya Walemavu ya Mpira wa Miguu (Tembo Warriors) kwa kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwezi Oktoba 2022 nchini Uturuki. Nitoe wito kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana kwa karibu na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kuwezesha maandalizi mazuri kwa timu zote mbili kuelekea mashindano hayo ya Dunia ili tukashindane na kuitangaza vema Tanzania.
85. Mheshimiwa Spika, mwisho kwa upande wa michezo niwapongeze sana Dar Young Africans (Wananchi) kwa kuibuka vinara wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2021/2022. Hongereni sana wananchi, mmekuwa na msimu mzuri sana na mmestahili kuibuka mabingwa. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa matukio yaliyonivutia wakati wa shamrashamra za Ubingwa wa wananchi ni kitendo chao cha kukumbuka kuitangaza Tanzania kupitia Royal Tour na kuhamasisha ushiriki wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kama ambavyo klabu ya soka ya Simba ilivyoanzilisha kuitangaza Tanzania kwenye medani za soka za kimataifa kupitia jezi zao kuandikwa VISIT TANZANIA. Niendelee kutoa wito kwa vilabu na makundi ya watanzania wanaosafiri nje kuhakikisha wanatumia jezi zetu zenye kubeba jumbe au ajenda za kitaifa kwani jukumu la kuitangaza Tanzania na ajenda zake za kitaifa ni letu sote.
HITIMISHO
86. Mheshimiwa Spika, ninapoelekea kuhitimisha hotuba yangu, niwatakie safari njema Waheshimiwa Wabunge wenzangu mnaporejea majimboni kwenu. Niwaombe mtakapokuwa huko majimboni muwaeleze wananchi mambo yaliyojiri hapa Bungeni wakati wote wa Mkutano wa 7 wa Bunge hili la 12, matarajio yetu kwao na kuwasihi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita kwenye jitihada zake za kuwawekea mazingira wezeshi ya kujikwamua kiuchumi.
87. Mheshimiwa Spika, niwashukuru pia, watendaji wa Serikali ambao weledi na ufanisi mkubwa waliouonesha umekuwa chachu katika kufanikisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu. Vilevile, niwashukuru wanahabari kwa kufikisha habari za Mkutano huu kwa wananchi. Kipekee, nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa huduma wanazozitoa kwa washiriki wa Bunge hili bila kuwasahau madereva waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa bungeni. Pia, nimshukuru Katibu wa Bunge na Watumishi wote wa Bunge kwa huduma nzuri mliyotupatia ambayo imetuwezesha kutekeleza majukumu yetu vizuri kwa kipindi chote cha miezi mitatu. Ninawatakia safari njema.
88. Mheshimiwa Spika, tunatarajia kwamba tarehe 10 Julai, 2022 kutegemea mwandamo wa mwezi, kutakuwa na sikukuu ya Eid El Hajj. Nitumie fursa hii kuwatakia ndugu zetu Waislamu na Watanzania wote nchini maadhimisho mema ya sikukuu hiyo.
89. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu liahirishwe hadi tarehe 13 Septemba 2022 siku ya Jumanne, saa tatu kamili asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu Jijini Dodoma.
90. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.