NA INNOCENT KANSHA-Mahakama
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kanda ya Dodoma, Mhe.Gerson Mdemu amewasisitiza Wahasibu na Wakaguzi wa ndani kutumia taaluma, maadili, miongozo, sera na sheria kurahisisha utelelezaji wa dira ya Mahakama inayohusu Upatikanaji wa Haki kwa Wakati na kwa Wote.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Gerson Mdemu akisisitiza jambo wakati wa kufunga mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani yalifanyika kwa siku tano katika Ukumbu wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma siku ya Juni 3,2022.
Akifunga mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani yalifanyika kwa siku tano katika Ukumbu wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma siku ya Juni 3,2022 Jaji Mdemu alisema, dira hiyo haiwezi kutekelezeka iwapo mifumo ya kihasibu waliyojifunza haitaondoa usumbufu kwa wadaawa kufanya malipo mbalimbali ya usajili wa mashauri na nyaraka za kimahakama kwa ufanisi, kulipa mirathi kwa wakati na watumishi wa ndani kulipwa stahiki zao bila usumbufu na kucheleweshwa.
“Pengine jambo la msingi ambalo mnatakiwa kulifahamu na kupitia mafunzo haya mmelifahamu ni kuwa upatikanaji wa haki kwa wakati na kwa wote haliwahusu maafisa wa Mahakama tu, bali hata ninyi mnahusika kwa asilimia mia moja katika utoaji wa huduma ya haki unaomlenga mwananchi na hivyo tukakatimize kwa vitendo,”aliongeza Jaji Mdemu.
Sehemu ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wakifuatilia mada ya Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2005 wakati wa mafunzo hayo yalifanyika kwa siku tano katika Ukumbu wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma.
Mhe. Mdemu akatoa rai kwa Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani kutumia ujuzi walioupata katika mafunzo hayo kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutatua changamoto za utoaji wa huduma za kihasibu ili kurahisisha na kuondoa usumbufu kwa wadaawa wanaowapa huduma, kwani TEHAMA ndiyo msingi wa kurahisisha upatikanaji wa huduma, kwa kuwa ninyi ndo mmefunzwa kuhusu matumizi ya hiyo mifumo basi msiende kuwa msiwe kikwazo cha utoaji huduma bora kwa wadaawa.
Sehemu ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wakifuatilia mada ya Mpango Mkakati wa Mahakama awamu ya pili wakati wa mafunzo hayo yalifanyika kwa siku tano katika Ukumbu wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma.
"Mahakama ya Tanzania inanuwia kuwa na maamuzi bora ya kimahakama ambapo imejiwekea malengo ya kukuza uelewa wa misingi ya taaluma ya kisheria na kuongeza ujuzi kwa watumishi wa mahakama. Katika kutekeleza malengo hayo, Mahakama imejiwekea mkakati wa kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama wa ngazi zote. Mmejengewa uwezo kwenye eneo lenu la kihasibu. Sasa hakutakuwa na kisingizio cha kuchelewesha huduma, hususani masuala ya mirathi ambayo yanahitimisha maamuzi yanayotolewa na Mahakimu na Majaji"', aliongeza Jaji Mfawidhi
Sehemu ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wakifuatilia mafunzo hayo.
Kuhusu mada zilizofundishwa Jaji Mdemu alisema maeneo yote yaliyofundishwa na wawezeshaji ni muhimu sana na yanahusu utekelezaji wa majukumu yao kama Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani kitaaluma na kimaadili. "Mmepewa nyenzo muhimu za utekelezaji kwenye maeneo mengine yaliyo nje ya taaluma yenu lakini hayaepukiki katika kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu katika kutoa huduma ya kihasibu. Mlikuwa na majadiliano mbalimbali ambayo yaliwawezesha kubadilishana uzoefu katika kazi zenu, mkayatumie yote mliyoyapata katika kufanyia kazi,"alisema Jaji Mdemu.
Sehemu ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani wakifuatilia mafunzo hayo. (Picha na Innocent Kansha - Mahakama).
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 ambapo katika Tunu ya Tano kuhusu weledi, Mahakama itatekeleza majukumu ya utoaji haki kwa umahiri na ufanisi.
Aidha, ndani ya Mpango Mkakati huo, katika nguzo ya kwanza inayohusu utawala, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, moja ya lengo ni kuwajengea uwezo watumishi wa ngazi zote.