NA DIRAMAKINI
SERIKALI kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya wanatekeleza Ujenzi wa Mfumo rahisi wa Maji taka kwenye makazi ya miinuko unaotekelezwa Bilioni 3.8 unaosaidia kuhifadhi maji taka kwenye matanki maalum na kuyatibu badala ya kumwaga kwenye Ziwa Victoria kama ilivyokua awali.
Hayo yamebainika Juni 7, 2022 mtaa wa Igogo -Sahara wakati wa ziara
ya Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akiambatana na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa alipokua akikagua Miradi ya
Maendeleo wilayani Nyamaga pamoja na kusikiliza na kutatua kero za
wananchi.
Vilevile, kupitia mradi huo kaya 122 zimeundiwa mfumo wa maji safi
na umewezesha ujenzi wa njia maalum za kupanda na kushuka kwenye mitaa
hiyo ambapo baada ya ukaguzi wake Mhe Mkuu wa Mkoa ameridhishwa na mradi
huo na amewapongeza watekelezaji wa mradi huo wa kisasa wenye ubunifu.
Vilevile,Mkuu
wa Mkoa ametoa wito kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri
ya Jiji la Mwanza kutoa elimu ya biashara kwenye vikundi vyote
wanavyowakopesha fedha kutoka makundi ya Wanawake, Vijana na wenye
ulemavu kwenye Halmashauri hiyo ili kuweka uhai wa vikundi
wanavyokopeshwa.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito huo kwenye Mradi wa
kikundi cha Vijana watano cha Yuoth Box Media kilichokopeshwa Milioni 49
mwaka 2021 ambacho kwa sasa kimekuza mtaji hadi kufikia thamani ya
Milioni 81 huku kikimiliki bidhaa za Habari kupitia Chaneli za mtandaoni
za Yu box Tv na Yu box Studio.
"Hawa wanafanya
vizuri ila mimi nimekuja kuona kama kikundi kina afya, je wana taarifa
za mapato na matumizi ya kikundi, wana vitabu vya fedha na wana
utaratibu wa kupima maendeleo ya kikundi chao, hapo lazima tujiulize na
Maafisa Maendeleo hiyo ndio kazi yetu kuwajengea uwezo", amesema.
Aidha,
Mkuu wa Mkoa amekagua Ujenzi wa Barabara ya Hesawa-Yatch Makaburini,
Tilapia -Vickfish yenye urefu wa Mita 650 liyotekelezwa kwa zidi ya
Milioni 348 na ameagiza kurekebisha dosari ndogo kwenye kingo za
barabara hizo na kusafisha mazingira.
Akiendelea na ziara yake Mhe Mkuu wa Mkoa ametoa pongezi kwa ujenzi wa Mradi wa vyumba 6 vya madarasa kwa mfumo wa ghorofa katika shule ya Sekondari Mkuyuni unaotekelezwa kwa Milioni 310 utakaosaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi kutoka 85 hadi 52 kwa darasa kwani madarasa hayo yatachukua wanafunzi 900.
Baada ya kukagua uhai wa Vilabu vya kupambana na rushwa na dawa ya kulevya katika shule ya msingi Nyegezi msafara wa Mhe Mkuu wa Mkoa ulifika kwenye Mradi wa Anuani za Makazi katika Mtaa wa Kisese kata ya Mkolani.
Kabla ya kukagua ujenzi wa jengo la Benki ya CRDB tawi la Buhongwa wenye thamani ya Milioni 500, Ujenzi wa Kituo cha Afya Bulale kata ya Buhongwa wenye thamani ya Milioni 500 umehitimisha ukaguzi wa miradi wilayani Nyamagana ambapo Mhe. Mkuu wa Mkoa amesisitiza ukamilishaji wa mradi huo kwa wakati ili uanze kuwahudumia zaidi ya wananchi elfu 5 wanaokusudiwa.