NA MARY MARGWE
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022, Sahili Geraruma ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara kwa uwajibikaji wake katika kusimamia kujengwa miradi yenye viwango, ambapo jumla ya miradi mitano yenye thamani ya shilingi bilioni 1.8 iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru imepita yote.
"Fedha za Serikali, wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo zimekwenda kihalali Kiteto, hivyo hongereni sana Kiteto mmeupiga mwingine hadi mmepitiliza,"amesema.
Kufuatia hilo Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Geraruma alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, John Nchimbi kwa uwajibikaji wake akishirikiana na wataalam wake, huku pia akimpongeza mkuu wa wilaya hiyo, Mbaraka Batenga kwa usimamizi wa miradi hiyo pamoja na madiwani.
"Mkurugenzi Mtendaji nikupongeze sana kwa juhudi kubwa unazoendelea nazo katika kuhakikisha miradi yote tuliyoipitia imesimama kikamilifu,yaani kiufupi Kiteto mmeupiga mwingi hadi mmepitiliza, mkuu wa wilaya hongereni sana endeleeni kushikamana kikamilifu ili kuweza kufikia malengo mliyojiwekea, miradi tumeipitia yote na imekidhi vigezo, japo kuna dosari ndogo ndogo naomba mzifanyie kazi," alisema Geraruma.
Aidha, alisema miradi inapokuwa inajengwa kwa viwango hivyo inawatia moyo hata waliotoa pesa wanapata nia ya kuendelea kuchangia miradi mwingine mbalimbali ya maendeleo inayoendelea katika maeneo mbalimbali, "hivyo endeleeni na juhudi hizo".
Aidha kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya hiyo, Mbaraka Batenga alisema, Mwenge wa Uhuru ulitembelea, jumla ya miradi ipatayo mitano yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.8.
Batenga alisema miradi hiyo ilzindua na kuweka jiwe la Msingi katika miradi mitano (5) ya maendeleo ambayo yamejengwa katika kipindi cha mwaka mmoja 2021/2022.
"'Ujenzi wa Kituo cha Afya Tarafa ya Olboloti-Kijiji cha Mwanya Kata ya Njoro umegharimu sh.500,000,000, ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Engusero Kata ya Namelock umegharimu sh.milioni 600, ujenzi Mradi Maji Kaloleni Kata ya Kaloleni umegharimu sh.milioni 400,"alisema Batenga.
Mbali na miradi hiyo aliitaja miradi mwingine kuwa ni Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Njia Panda Kata ya Namelock shilingi milioni 50,000,000 pesa za ziada pamoja na Ujenzi wa Mradi wa Hotel ya Kilimanjaro ya Puliza mradi wa mtu binafsi uliogharimu jumla ya sh.milioni 250.