Maafisa rasilimali watu wa Serikali, sekta binafsi kukutana jijini Mwanza

NA DIRAMAKINI

MKUTANO Mkuu wa Pili wa Umoja wa Maafisa Rasilimali Watu na Utawala (HRAOT) utafanyika jijini Mwanza, Juni 15, mwaka huu na kuwashirikisha maofisa 400 kutoka serikalini na sekta binafsi.
Mjumbe wa Kamati ya Tendaji ya HRAOT,Monica Andrew amesema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa mkutano huo unalenga kujadili changamoto za kiutendaji na utawala zinazoikabili kada hiyo na kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha utendaji.

“Mkutano huu wa pili wa mwaka unahusisha maofisa rasilimali watu na utawala wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi,ni njia ya uendeshaji wa taasisi ili kuisaidia serikali na kuwaunganisha watumishi kazi ambayo si rahisi,tunatakiwa kuwasaidia waajiri malengo yao yaende sawa sawa na kuwakumbusha watumishi haki na wajibu kuwa vinakwenda sambamba,”amesema Monica.

Amesema, katika mkutano huo watajadiliana kuhusu utendaji wao wa utumishi ili kurahisisha kufikiwa kwa haki na wajibu wa watumishi na kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuliletea taifa maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, akizungumzia mkutano mkuu huo wa HRAOT kufanyika mkoani humu na kuwepo kwa Maofisa Rasilimali Watu na Utawala 400 ni fursa kwa kada hiyo,wadau wa maendeleo na wafanyabiashara.

Amesema, mkutano huo unalenga kubadilishana uzoefu wa utendaji na kuishauri serikali namna bora ya usimamizi wa watumishi wa umma na binafsi kuhusu utendaji kazi bora wa kuzingatia weledi wenye tija.

“Nimefarijika kwa uamuzi wa kuuleta mkutano mkuu huu wa pili wa Umoja wa HRAOT hapa Mwanza ambao utafanyika Juni 15 hadi 17 mwaka huu,ukiwa na kauli mbiu; “Uwepo wa Takwimu za uhakika ni Msingi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Mali,Twendeni Tukahesabiwe kwenye Sensa ya Mwaka 2022,”amesema Mhandisi Gabriel.

Pia ametoa wito kwa Maofisa Rasilimali Watu na Utawala wote waliopo Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa,Mashirika ya Umma, Wakala wa Serikali na Taasisi Binafsi nchini kuhudhuria mkutano huo kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa bila kukosa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news