NA DIRAMAKINI
MADEREVA Bajaji, Bodaboda, mama lishe na wafanyabiashara ndogo ndogo wanaofanya shughuli zao eneo la Morocco Hoteli Kata ya Magomeni Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wamemwangukia Diwani wa Kata hiyo, Nurdin Butembo, baada ya kutakiwa kuondoka mara moja ili kupisha mradi wa mabasi ya mwendokasi kufanya shughuli zake.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam mbele ya Diwani Butembo waliempigia simu kwa ajili ya kumuomba kwenda kuwasikiliza wafanyabiashara hao walilalamika wakidai kuwa, hawana sehemu ya kufanyia shughuli zao hivyo wanamuomba kiongozi huyo kuwasaidia kwani taarifa hiyo ya kuondoka mara moja ilikuja ghafla.
Katibu wa Umoja wa Madereva Bajaji Morocco Hotel (UMABAMO), Nurdin Salim akizungumza kwa niaba ya wenzake waliokusanyika katika eneo hilo la Kituo cha Mwendokasi mbele ya Diwani huyo amesema kuwa, awali walisajili kikundi lakini wakaambiwa kuwa wakae kwa muda ili wenyewe wakihitaji eneo lao (DART) madereva hao na wafanyabiashara basi waondoke.
"Mhe. Diwani sisi hatukatai kuondoka, hapana hilo liko wazi lakini kinachotuuma hatujapewa muda wa kujiandaa hivyo basi tunakuomba angalau tujibanze huku pembeni ambapo huduma zitakuwa hazifiki kwani tumeambiwa tuondoke haraka yaani taarifa tumeletewa Mei 30, 2022,"amesema Katibu huyo.
Mtendaji Kata wa Mtaa wa Makuti 'A', Richard Yomo amesema kuwa, awali walipokea taarifa kutoka DART inayoelekeza kutaka kutaka wafanyabiashara na madereva hao kuondoka eneo hilo mara moja kwa madai kuwa Kituo hicho kinaanza kufanya kazi muda si mrefu.
"Baada ya tangazo hilo kutoka DART na sisi tuliwapa taarifa wahusika kwamba wenye eneo lao wanalihitaji hivyo waondoke ndipo Viongozi wa UMABAMO walipoamua kumuita Mhe. Diwani ili aweze kuwasikiliza na kutolea majibu malalamiko yao," amesema.
Diwani Butembo baada ya kusikiliza malalamiko hayo amesema, "mimi nimesikiliza malalamiko, maombi lakini pia na ushauri kwa kila kikundi,"amesema na kuongeza;
"Lakini nyote mnajua kwamba walisema wakitaka eneo lao inabidi muondoke maana yake hata wangekuja sa moja asubuhi wakawambia sa sita mchana msiwepo ingebidi mtii kwani taarifa mnayo,".
Aidha, alisema kutokana na taharuki ya watu hao ametoa maelekezo kwa uongozi wa Serikali za Mtaa pamoja na kumpa maelekezo Mtendaji kwamba akae na wajumbe wa Mtaa ili kupata muhafaka na badaye wampelekee mrejesho.
"Maana yangu ni kwamba wajumbe wa mtaa na Mtendaji wakikaa na kuzungumza tutapa muhafaka na kujua tunaelekea wapi katika kutatua jambo hili lakini pia kwa mama lishe hawatakiwi kukaa mbele ya nyumba au fremu ya biashara ya mtu," amesema Diwani Diwani Butembo.