NA FRESHA KINASA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara limegomea ongezeko la tozo ya Shilingi 100 kwenye kila kilo ya samaki iliyopendekezwa kuongezeka katika tozo ya sasa inayotozwa Shilingi 100 ili iwe Shilingi 200, na badala yake baraza hilo limetaka tozo iliyopo kwa sasa shilingi 100 iendelee kutozwa kuwapa ahueni wafanyabiashara wa samaki pamoja na wananchi.
Uamuzi huo umefanyika Juni 2, 2022 katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Kata ya Mugango wilayani humo ambapo pia Madiwani hao walitaka usimamizi madhubuti ufanywe katika kukusanya mapato ya vyanzo vingine na sio kuongeza tozo ya samaki.
Ambapo makisio kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 walipanga kukusanya ushuru wa mialo (samaki) na maegesho Shilingi milioni 684.2 lakini kiasi kilichokusanywa kuanzia Julai hadi Machi 2021/ 2022 ni shilingi milioni 446.9.
Pendekezo la ongezeko la Shilingi 100 katika tozo ya sasa inayotozwa Shilingi 100 liliwasilishwa katika kikao hicho na kujadiliwa na madiwani kufuatia Kamati ya Fedha na Mipango kupendekeza baada ya kutuma Mwanasheria katika wilaya ambazo zinajishughulisha na uvuvi ikiwemo Wilaya ya Ukerewe, Muleba na Rorya na kuleta mapendekezo hayo ili kuongeza mapato ya halmashauri hiyo.
Diwani wa Kata ya Nyakatende, Malele John amesema kuwa, pendekezo la ongezeko la Shilingi 100 katika tozo ya sasa inayotozwa 100 itawaumiza wananchi hivyo tozo iliyopo ndiyo inapaswa kuendelea kutozwa.
"Hoja ya ongezeko la tozo Shilingi 100 ambayo imeletwa itasababisha utoroshaji wa Samaki bila kulipiwa kodi. Hoja sio ongezeko la tozo bali Usimamizi thabiti ufanywe na menejimenti tukiongeza tozo hii tutazidi kuwaumiza Wananchi wetu,"amesema Mheshimiwa John.
Naye Diwani wa Kata ya Etaro, Emmanuely Majiga amesema kuwa, bei ya samaki imeshuka, hivyo kitendo cha kuongeza tozo ni kuwafanya Wafanyabiashara na Wananchi wapate tabu kwani soko la samaki limekuwa likibadilika badilika mara kwa mara hasa katika soko la dunia.
"Sioni sababu ya kuongeza mzigo wa tozo kama huko nyuma tulishindwa kutoza Shilingi 250 iliyokuwepo tukaitoa naomba tuendelee kutoza Shilingi 100 bila kuongeza. Kuna vyanzo vingi vya mapato ikiwemo migodi, masoko na maeneo mengine visimamiwe vyema kuongeza mapato ya halmashauri,"amesema Jogoro Malyango Diwani wa Kata ya Suguti.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Magange Mwita amesema kuwa pendekezo hilo la tozo ni kutaka kuongeza mapato ya halmashauri hiyo. Ambapo pia kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 kila robo watapaswa kupeleka shilingi 200,000 kwenye kila kijiji na kata hivyo lazima wawe na mapato ya kutosheleza.
"Bajeti yetu imeongezeka, mwaka wa fedha wa 2021/2022 ilikuwa shilingi Bilioni 1.7 kwa sasa kuna ongezeko la zaidi ya shilingi milioni 200 imefikia Bil.1.9 kwa mwaka wa fedha 2022/ 2023 baada ya mapitio ya bajeti tumeamuliwa makisio kuwa bil.1.9 kwa mapato ya vyanzo vya ndani ya Halmashauri lazima tukusanye kwa asilimia 100. Katika hali ya sasa lazima tuongeze mapato kwa sababu gharama zimeongezeka na matumizi ya gharama za uendeshaji,"amesema Mwita.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Charles Magoma amesema jambo hilo lirudi upya kwenye menejimenti likachakatwe upya waje na mapendekezo mengine yatakayoishawishi Kamati ya Fedha na Mipango na baraza hilo kuweza kuongeza tozo isiyoumiza wavuvi na wananchi.
"Mkurugenzi muende mkachakate upya suala hili zamani tulitoza Shilingi 250 lakini ilileta shida kweli. lazima mzani ubalance mvuvi asiumie sana." amesema Charles Magoma.
Abeli Mafuru ni Diwani wa Kata ya Bulinga amesema kuwa, leseni ya mtumbwi wa kasi ni Shilingi 115,000 na mtumbwi wa mashine ni Shilingi 138,000 hivyo iwapo tozo ikiongezeka italeta maumivu makubwa kwa wananchi na wafanyabiashara wa samaki kwani maeneo mengine gharama ya leseni iko chini ikilinganishwa na Musoma Vijijini.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Halfan Haule akizungumza katika kikao hicho cha baraza amesema kuwa, Msingi wa Jambo hilo lianzia kwenye kamati ya usalama ambapo amesema Halmashauri ya Musoma inatoza tozo ndogo ikilinganishwa na maeneo mengine. Amesema, katika Wilaya ya Bunda tozo ni Shilingi 300 kwa kilo, Manispaa ya Musoma Shilingi 300 kwa kilo, Rorya Shilingi 300 kwa kilo.
"Kwanza nipongeze utafiti uliofanywa na Mwanasheria juu ya ongezeko la tozo katika maeneo ambayo shughuli za uvuvi zinafanywa. Pia niwapongeze Madiwani ambao nanyi mmetoa mapendekezo yenu, samaki ndicho chanzo cha uhakika katima halmashauri yetu Halmashauri hii ya Musoma inatoza kiwango cha chini sana maamuzi ni yenu Madiwani kuamua juu ya ongezeko la tozo hii kwa sababu fedha hiyo inakuja pia kwenu kufanya shughuli za maendeleo kwa manufaa ya Wananchi," amesema Dkt.Haule.
Aidha, akitoa salamu za serikali Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dakt. Halfan Haule amempongeza Rais wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za maendeleo katika kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo. Huku akiwaomba wadiwani kuwaandaa Wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya watu na makazi mwezi agosti mwaka huu.