NA FESTO SANGA-Mahakama
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa imeanza kutekeleza kwa vitendo agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alilolitoa hivi karibuni alipokuwa katika ziara ya Mahakama, Kanda ya Tanga, la kutambua na kuweka vibao vya anwani za makazi katika majengo ya Mahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (kulia) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe Gadiel Mariki (kushoto) wakifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa zoezi uwekaji wa anauani za makazi Kanda ya Kigoma.
Hayo yalibainishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa zoezi la kuweka anuani za makazi katika majengo ya mahakama lililofanyika katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma hivi karibuni.
Katika hafla hiyo, Mhe. Mlacha alisema kuwa zoezi hilo litazifanya Mahakama zilizopo katika Kanda yake kutambulika kwa urahisi na wateja, hivyo kuwezesha utoaji wa huduma za hai kwa wakati.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akiwapatia watumishi kibao na namba kwa ajili ya Mahakama ya Wilaya ya Kasulu katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika hivi karibuni.
Naye Mtendaji wa Mahakama katika Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka alieleza kuwa pamoja na kutekeleza zoezi la anwani za makazi kila Mahakama imeanza utekelezaji wa kutumia anwani mpya kwenye barua za kiofisi.
Hata hivyo alieleza kuwa zoezi la utambuzi na uwekaji wa vibao vya namba na anwani halijakamilika kwenye Mahakama za Mwanzo nane zisizofanya kazi kutokana na uchakavu mkubwa wa majengo hayo kiasi cha kutotambuliwa na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mahakama 2 zinazofanya kazi kwa kutumia majengo ya maafisa Tarafa ambazo ni Manyovu na Kasangezi. Alizitaja Mahakama hizo za Mwanzo ambazo hazifanyi kazi kama Nyavyumbu, Mgunzu, Kumsenga, Buhoro, Mnyegera, Mwayaya, Mgambo na Kagunga.
Watumishi wa Mahakama Kuu Kigoma wakiwa wameshikilia kwa furaha baadhi ya vibao vya Mahakama mbalimbali katika tukio la uzinduzi wa zoezi la uwekaji wa vibao vya anuani za makazi lililofanyika hivi karibuni.
Alibainisha kuwa jitihada zinafanywa kwa kushirikiana na Mamlaka husika kuzitambua Mahakama hizo, kupata namba za majengo, jina la barabara au mtaa na postikodi kwa urahisi wa uandaaji wa anwani za maeneo hayo ili kukamilisha zoezi kwa asilimia mia moja.