NA SOPHIA FUNDI
MAMEYA na wenyeviti wa halmashauri zote Mkoa wa Arusha wametakiwa kusimamia mapato ya halmashauri zao na kuona fedha zilizokusanywa zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ALAT Taifa,Elirehema Kaaya wakati akizungumza kwenye mkutano wa ALAT Mkoa wa Arusha uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
Bw.Kaaya alisisitiza mshikamano katika halmashauri kwa kujenga mahusiano mazuri kati ya waheshimiwa madiwani na CMT na kuepuka migogoro kati ya wenyeviti na Mameya na madiwani pamoja na watendaji wa halmashauri kwa mustakabali mwema wa halmashauri katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Amewataka viongozi wa halmashauri kujikita katika kuhakikisha halmashauri zao kupata hati safi za ukaguzi kwa kutekeleza miradi inayoendana na thamani ya fedha, hivyo aliwataka kusimamia vizuri matumizi ya fedha za serikali.
Kwa upande wake mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Arusha, Maxmilian Iranghe aliwataka wenyeviti na mameya kusimamia suala zima la usafi kwenye halmashauri zao kwa kuunga mkono juhudi za Rais katika kuhamasisha suala zima la utalii hasa ukizingatia mkoa wa Arusha kuwa lango la utalii ikiwemo na wilaya ya Karatu.
Baada ya wajumbe hao wa ALAT kutembelea miradi ya maendeleo katika halmashauri ya wilaya ya Karatu wameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kwa usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotengewa fedha na serikali ambapo thamani ya fedha ilionekana.
Walisema kuwa, wamejifunza mengi kutoka katika halmashauri hiyo wakati walipotembelea miradi ya maendeleo ikiwemo usimamizi mzuri wa fedha za miradi ambapo alisema kuwa ni Halmashauri chache Sana kutekeleza miradi na kubaki chenchi.
"Kwa kweli Karatu mmefanya vizuri sana kusimamia fedha za serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni miradi mikubwa sana iliyotumia fedha nyingi, lakini fedha hizo kwenye baadhi ya miradi inaonyesha kubakiwa na chenchi baada ya kukamilika mradi.Hongereni sana Karatu tuwaige wenzetu na tuwapongeze kwa kazi nzuri,"amesema Iranghe.