NA JOHN MAPEPELE
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe, Mohamed Mchengerwa akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi mekutana na Balozi wa Marekani hapa nchini leo Juni 8, 2022 jijini Dar es Salaam na kujadili masuala mbalimbali ya sekta ya michezo na sanaa ikiwa ni pamoja na ujio wa msanii mashuhuri wa uchoraji,Ashley Collins hapa nchini.
Mhe.Mchengerwa amesema, viongozi hao wamekubaliana kuendeleza malengo ya Royal Tour kwa kushirikiana zaidi kwenye kuendeleza sekta za sanaa na michezo ikiwemo kuendeleza filamu za hapa nchini za “Swahiliwood” ili ziwe katika kiwango cha Kimataifa kama zile za nchini Marekani kwa kupata walaam ambao watasaidia katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa miswada (script).
Aidha, amesema eneo jingine ambalo limejadiliwa ni pamoja na kutoa mafunzo maalum katika eneo la haki miliki na hakishiriki kwa kazi mbalimbali za wasanii ikiwa ni pamoja na tuzo za muziki na kwa upande mwingine amesema wamejadili namna ya kushirikisha wataalam kwenye program maalum ya kuibua vipaji vya wasanii na wanamichezo ya mtaa kwa mtaa.