Mbaroni Dar kwa kufanya biashara ya ngono mitandaoni, kujifanya mawakala wa Freemason

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kwa kushirikiana na timu maalum ya kuzuia na kupambana na uhalifu mtandaoni, imefanya oparesheni maalum kuanzia Mei 18,2022 hadi Juni 26,2022 na kuwakamata Marry Samson Sibora maarufu Asha Zungu ( 23) mkazi wa Sinza Mugabe na Zainabu Yahaya Omary maarufu official Manka (23) mkazi wa Buguruni wakituhumiwa kwa usambazaji wa picha za ngono.

Sambamba na kuuza mwili kwa njia ya mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook, WhatsApp, Tinder na Exotic tz.

Kamanda Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema, watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na taratibu za kisheria zinakamilishwa ili wafikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo.
Operesheni hiyo iliyofanyika kati ya Mei 18 hadi Juni 26 ilifanyika pia katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro ambapo watuhumiwa wengine walikamatwa huko.

“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kisheria, linatoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na uhalifu kwa njia ya mtandao na njia nyingine, kuwa Serikali na vyombo vyake imejipanga kupambana na uhalifu wa aina yoyote, na wahalifu popote walipo watafuatwa, kukamatwa na kupelekwa mahakamani.

“Aidha, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa Watanzania wote kutumia mitandao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na kuwa waangalifu na vitendo vya utapeli, ikiwemo kuchukuwa tahadhari wakati wa kutuma pesa au kufanya biashara katika mitandao ili kuepuka kutapeliwa, pia watu wajiepushe kufanya biashara haramu mitandaoni kama vile za kuuza mili na ngono,"amesema.

Wakati huo huo amesema, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu zaidi ya 20  kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya utapeli kwa njia ya mtandao.

Kukamatwa kwa watu hao ni matokeo ya operesheni hiyo maalum iliyofanywa na kanda hiyo kwa kushirikiana na timu maalumu ya Kuzuia na Kupambana na Uhalifu wa Mtandaoni.

Kamanda Jumanne Muliro amesema, waliokamatwa ni watuhumiwa waliokuwa wakijifanya wakuu wa shule, waganga wa kienyeji, ndugu wa waathirika, wahudumu wa makampuni ya simu au mawakala wa Freemason.

Amesema, watuhumiwa hao huwatumia watu ujumbe mbalimbali kupitia namba tofauti za simu na kujifanya wanania ya kusaidia watu badala yake huishia kuwaibia.

Miongoni mwa waliokamatwa ni Julius Simon Mwabula (20) ambaye ni mkazi wa Ifakara Morogoro sambamba na wenzake 22.

Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na vifaa mbalimbali ambavyo wanavitumia kufanya uhalifu huo ikiwemo hivyo ni kama Kompyuta mpakato 2, kompyuta ya mezani 1, simu za aina tofauti 28, flash 2, modem ya mitandao yote na kadi za simu za mitandao mbalimbali zaidi ya 50.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news