Mbaroni kwa kufukua kaburi la marehemu mtoto wake, baada ya kuchoka aliwatumia wanafunzi kwa ujira wa 10,000/-

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia, ndugu Tanga Thadeo (30) mkazi wa Kitongoji cha Kasisiwe Manispaa ya Sumbawanga kwa tuhuma za kuwatumia wanafunzi wa darasa la nne na sita wa Shule ya Msingi Kasisiwe kufukua kaburi la marehemu mtoto wake akidai kuwa anataka kumfufua kwa kuwa anaamini alikufa katika mazingira ya kishirikina. 
Tukio hilo lilitokea Juni 21, mwaka huu majira ya saa 9 mchana ambapo mtuhumiwa alikwenda katika makaburi ya Kasisiwe kwa lengo la kufukua kaburi la mtoto wake aitwaye Martin Tanga (2) aliyefariki siku ya Juni 16, mwaka huu na kuzikwa siku iliyofuata katika makaburi hayo. 

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Theopista Mallya amesema kuwa baada ya mtuhumiwa kufukua kaburi hilo na kuchoka aliamua kuacha na kwenda kuwaita wanafunzi wa kiume wa Shule ya Msingi Kasisiwe waliokuwa wakicheza mpira karibu na makaburi hayo kisha kukubaliana nao wamsaidie kufukua kwa ahadi ya kuwalipa shilingi 10,000.

Akisimulia namna walivyofukua kaburi hilo mmoja wa wanafunzi hao jina limehifadhiwa alisema kuwa, kabla ya kuanza kufukua mtuhumiwa aliwataka kwanza wasali, ambapo yeye aliongoza sala na walipo maliza ndipo zoezi hilo likaanza. 

Baada ya kuchimba na kufukua kwa muda mrefu walilifikia jeneza ambalo mwili wa marehemu ulikuwemo na mtuhumiwa aliwataka waache, na aliingia ndani ya kaburi hilo na kulitoa jeneza na kisha kulifunga mgongoni kwa kutumia shati alilovaa akatoka, akawapa wanafunzi hela waliyokubaliana na kisha kuondoka.

Kamanda Mallya amesema, baadaye wakazi wa kitongoji hicho waligundua kuwa kuna kabuli limefukuliwa na mwili wa marehemu umechukuliwa ndipo walipotoa taarifa kwenye serikali ya mtaa na kituo cha polisi ndipo uchunguzi ulipo anza na kumbaini muhusika wa tukio hilo kisha kumakamata kutokana na vitendo alivyo fanya.

Amesema kuwa, baada ya polisi kumkamata na kumuhoji alikiri kufukua kaburi hilo na kuchukua maiti ya mwanaye na kudai kuwa alikua anataka kwenda kumfufua kwakua yeye binafsi haamini kama kifo alichokufa ni cha kawaida kwani anaamini kilitokana na mazingira ya kishirikina.

Kamanda huyo wa polisi amesema kuwa, mtuhumiwa anashikiliwa kwa kufukua kaburi kwani ametenda kosa la jinai, kwani hata kama alitaka kufukua angefuata sheria ikiwemo kuomba kibali lakini ni kosa kujiamlia kufukua yeye mwenyewe tena amewashirikisha wanafunzi kufukua kabuli hilo, hivyo atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika hivi karibuni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news