NA DIRAMAKINI
MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Mheshimiwa Omary Kumbilamoto amempongeza Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii nchini, Nabii Dkt. Joshua Aram Mwantyala kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo,huku akisema huo ni mpango kutoka kwa Mungu.
"Nikupongeze kwa nafasi hiyo uliyoipata...niliona hali ile siku ile nilikuwa sina mashaka. Yuko kiongozi mmoja akaniambia yeye atakuwa Rais amepiga kampeni hadi saa tisa usiku, nikambana Kaka yangu Siza akasema Mungu kuna mtu kashamtawaza kuwa Mfalme hakujitaja yeye,"amesema Meya.
"Baada ya matokeo nikamuuliza imekuwaje akasema haya mambo yamekwisha kuwa kama siasa rafiki yangu, wajumbe wamenishugulikia kumbe kasahau kile kisa cha Daudi alivyopata ufalme.
"Kwa sababu Mjumbe yule kutoka kwa Mungu alipofika kwa mzee Yese kuna mwanaye yule wa kwanza ndiye alijiandaa na watu wote wa Mji wakajua huyu ndiye atakuwa Mfalme baada ya mzee.
"Lakini, Mungu akasema nenda kwenye nyumba ya mzee Daudi yupo mfalme atatoka kwenye nyumba ile kwa hiyo yule aliyejiandaa hakuteuliwa akaja wa pili hakuteuliwa, wamejikuta nyumba nzima hakuna hata mmoja ambaye ni mteule mwisho wa siku Mjumbe ambaye Mungu amemtuma kwenda kwenye ile nyumba anasema sasa itakuwaje...Muulize huyo mzee ana mwanaye mwingine? Ndio mzee Yese akasema yupo mtoto anaitwa Daudi anachunga mleteni, kuletwa ndiye huyo huyo." amesema Meya.
Aidha, Meya huyo ametoa rai kwa Watanzania kumpongeza na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake njema ya kufuta ada ya kidato cha tano na sita.
"Tukio ambalo lilitakiwa kufanyika miaka ya 1970 na 1980 huko maana yake sasa mtoto wa mama ntilie, boda boda anasoma kuanzia Nursary hadi form six bure,"amesema Meya.
Kwa upande wake Rais wa Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania, Nabii Dkt. Joshua Aram Mwantyala amesema, anamshukuru Mungu kwa kuendelea kumtumia kwa viwango vya juu katika huduma na kuwa wakili bora wa Serikali ya Mbinguni.
"Ukitaka kuperfom (kufanya) miujiza ya kiungu lazima unaposimama mbele ya mtu unayemhudumia uwe huna dhambi. Kipofu mmoja aliongea kidogo tu, lakini amekuwa maarufu kuliko wote katika Biblia..alisema Mungu hawezi kumtumia mwenye dhambi.
"Kama Rais wa Mitume na Manabii kwa kizazi tulichonacho ipo miujiza mingi feki watu wanajitahidi hawaoni matokeo baadaye wanatengeneza wenyewe yaani unachonga mwenyewe muujiza. Mungu alinifundisha alisema leo nimepata faida kujipata nilikuwa sijajipata.
"Tangu nilipojipata sina hatia nimekuwa wakili bora sana wa Serikali ya Mbinguni popote ninaposimama Mungu ananitumia. Naona miujiza ya kushangaza sababu nasimama kama mtu asiye na hatia," amesema Nabii Joshua.
Tags
Habari