Mheshimiwa Kagaigai atoa maelekezo madeni ya milioni 400/- Same

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro,Mheshimiwa Stephen Kagaigai ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhakikisha madeni zaidi ya shilingi milioni 400 yanayotokana na mikopo iliyotolewa kwa vikundi vya wanawake,vijana na wenye ulemavu inarejeshwa ili fedha hizo zitumike kuwanufaisha wengine.

Utaratibu wa halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani uliasisiwa na Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17-2020/21) lengo ikiwa ni utoaji wa mikopo yenye gharama na masharti nafuu, utekelezaji ambao ulianza mwaka wa fedha 2018/19.

Mheshimiwa Kagaigai ameelekeza kurejeshwa kwa fedha hizo alipokuwa akizungumza katika kikao maalumu cha baraza la madiwani kilichoketi kupitia hoja mbalimbali za mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

"Halmashauri lazima mhakikishe mnatenga fedha za wanawake, vijana na wenye ulemavu, pamoja na fedha hizi kwamba zinatolewa kama mkopo ni lazima zirejeshwe, hizi fedha sio za kugawiwa ni fedha za mikopo, ukishaitwa mkopo ni lazima ujue unarejeshwa," amesema.

Amesema madeni yanayotokana na vikundi hivyo ni lazima yarejeshwe na wale wote waliochukua fedha hizo wanapaswa kuzirejesha ili ziweze kuwanufaisha wengine na kwamba hawahitaji kutumia migambo kuzirejesha fedha hizo.

"Hizi fedha zimetolewa ili ziweze kuwanufaisha wananchi na ni lazima wale waliochukua mikopo na hawajarejesha zirejeshwe kistaarabu sio kutumia migambo au RPC wakati hizi fedha zimetolewa na Rais kuwasaidia wananchi,"amesema Kagaigai.

Akizungumzia kuhusu madeni hayo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, Isaya Mngulu amesema, fedha hizo zilizokopeshwa ni nyingi na kwamba halmashauri hiyo inapaswa kuchangamka kukusanya madeni hayo.

"Hizi zaidi ya Sh400 milioni tulizokopesha na tunazodai ni nyingi na huenda serikali ikashindwa kutoa tena mikopo mpaka hizi fedha tunazodai zirejeshwe, katika hili mwenyekiti tuchangamke ili hizi fedha zirudi,"amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala mkoa huo, Willy Machumu amesema, madeni hayo yanatokana na baadhi ya watendaji kushindwa kutekeleza majukumu yao na kutoa majibu yasiyoridhisha kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) pindi anapofanya ukaguzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news