Msajili Mkuu:Tufuatilie Kipindi cha Sema na Mahakama ya Tanzania

NA MARY GWERA-Mahakama

MSAJILI Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma ametoa rai kwa wananchi kuendelea kufuatilia kipindi mubashara cha ‘Sema na Mahakama ya Tanzania’ kinachorushwa kupitia vituo vya televisheni vya ‘TBC’ na ‘ITV’ ili kufahamu taratibu na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama. 
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo katika picha) tarehe 10 Juni, 2022 ofisini kwake Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam. Mhe. Chuma ametoa rai kwa wananchi kufuatilia Kipindi cha Sema na Mahakama ili kupata uelewa wa masuala mbalimbali ya kisheria.

Akizungumza na Waandishi wa Habari tarehe 10 Juni, 2022 ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mhe. Chuma amesema kuwa programu maalum ya kutoa elimu kwa umma kupitia kipindi hicho imeanzishwa mahsusi kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kufuatia uelewa mdogo wa masuala ya sheria miongoni mwao. 

“Ndugu Wanahabari, mtakumbuka kuwa mnamo tarehe 17 Mei mwaka huu takribani mwezi mmoja sasa, Mahakama ya Tanzania ilianza kutoa elimu kwa wananchi kupitia kipindi mubashara kinachorushwa kupitia TBC na ITV hivyo tungependa wananchi wapate taarifa kuhusu taratibu mbalimbali za uendeshaji wa shughuli za Mahakama kupitia wazungumzaji ambao ni Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wanaoshiriki kutoa mada mbalimbali,” amesema Msajili Mkuu. 

Mhe. Chuma ametaja mada kadhaa ambazo zimekwishatolewa hadi sasa ambazo ni Mahakama ya Tanzania na Mpango wa Uboreshaji Huduma, Taratibu za Mirathi katika maendeleo ya familia na Haki ya Msaada wa kisheria katika Uendeshaji wa mashauri mahakamani. 
Msajili wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (kulia) akizungumza na Wanahabari (hawapo katika picha) alipofanya mkutano nao kwa ajili ya kuwajuza kuhusu maendeleo ya kipindi maalum cha Sema na Mahakama ya Tanzania. Ametoa kwa wananchi kuendelea kufuatilia mada mbalimbali zinatolewa na Maafisa wa Mahakama ili wapate ufahamu wa taratibu na huduma za Mahakama. Kushoto ni Katibu wa Msajili huyo, Mhe. Jovine Bishanga.

Ameongeza kuwa, kupitia kipindi hicho mada nyingine nyingi zitaendelea kutolewa ikiwemo uaandaaji, uandishi na utunzaji wa wosia, taratibu za kupata dhamana, Matumizi ya TEHAMA kuelekea Mahakama mtandao na kadhalika. 

“Mbali na kufahamu taratibu za kimahakama ni muhimu pia wananchi wafahamu uboreshaji unaofanyika mahakamani wenye lengo la kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi, kwa mfano kwa sasa Mahakama imepiga hatua katika matumizi ya TEHAMA, uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake na mengine mengi ambayo wananchi wanastahili kupata taarifa sahihi kuhusu Mhimili huu,” amesisitiza. 

Aidha, Mhe. Chuma amewakumbusha wananchi kuendelea kutumia namba ya simu ya Kituo cha Kutoa Taarifa cha Huduma kwa Mteja (Call Center) ambayo ni 0752500400, na baruapepe maoni@judiciary.go.tz ili kutoa maoni, malalamiko ili Mahakama ifanyie kazi kwa kuwa imeanzisha huduma hiyo kumuwezesha kila Mtanzania apate haki kwa wakati. 

Kipindi mubashara cha ‘Sema na Mahakama ya Tanzania’ hurushwa ‘ITV’ kila Jumanne kuanzia saa 12:30 jioni hadi saa 01:30 usiku, hali kadhalika kipindi hicho huruka 'TBC' kila Alhamisi kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 01:00 usiku.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news