NA FRESHA KINASA
MKUU wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Dkt.Halfan Haule amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutorubunika na kuuza vyakula vyao na mazao yao ya shambani kufuatia uwepo wa watu kutoka nchini Kenya ambao wamekuwa wakipita wakitafuta vyakula katika familia na mashamba yao waweze kununua.
Dkt.Haule amesema kuwa, mwaka huu hali ya upatikanaji wa chakula si ya kuridhisha hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kutunza akiba ya chakula walicho nacho na kukitumia kwa umakini mkubwa kwani mvua hazikuwa za uhakika.
Ameyasema hayo Juni 2, 2022 wakati akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la madiwani Halmashauri ya Wilaya hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki Muganga Wilaya ya Musoma.
"Mwaka huu ni mwaka wa njaa, mvua hazikunyesha kwa kiwango ambacho kingekuwa na manufaa makubwa wapo watu kutoka Kenya wamekuwa wakipita pita kununua vyakula kwa wananchi na mashambani, niwaombe wananchi wasiuze vyakula vyao bali watunze, nanyi Madiwani niwaombe muwasisitize Wananchi wazingatie hili,"amesema Dkt.Haule.
Aidha, amewaomba wananchi kuendelea kuzitumia mvua chache zinazonyesha kulima viazi na mazao mengine katika kujihakikishia uhakika wa ziada ya chakula katika familia zao.
Katika hatua nyingine, amewaomba madiwani kuwahimiza wananchi katika maeneo yao kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika mwezi Agosti 23, mwaka huu ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango yake ya maendeleo kwa wananchi.
Aidha, Dkt.Haule amesisitiza pia ushiriki wa wananchi wote katika jukumu la ulinzi na usalama katika maeneo yao ili kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea kufanyika kwa amani na utulivu sambamba na kufanya shughuli halali za maendeleo yao na taifa pia.