Mwanasheria Mkuu wa Serikali apendekeza njia bora inayowafaa Wanahabari Tanzania

NA DIRAMAKINI

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Mhe.Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (AG) amependekeza kuwepo na bodi ya wanahabari itakayosimamiwa na wanahabari nchini.
Amesema, chombo hicho ndicho kitachokuwa na wajibu wa kusimamia wanahabari na hata kuwashughulikia endapo watakwenda kinyume na maadili ya habari.

Jaji Dkt.Feleshi ametoa kauli hiyo leo Juni 13, 2022, ofisini kwake bungeni, jijini Dodoma alipokutana na wadau wa habari nchini.
"Sina tatizo, naona muwe na 'regulator', bodi yenu moja, ili mmoja wenu akienda kinyume na maadili (ya uandishi wa habari), mnamshughulikia nyinyi wenyewe," amesema Jaji Dkt.Feleshi.

Jaji Dkt.Feleshi ametoa kauli hiyo baada ya Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kumweleza kuwa, wanahabari wanapendekeza kuundwa kwa chombo kimoja kitakachosimamia wanahabari badala ya vyombo vinne kama inavyoelekezwa na sheria ya sasa.
Pia Balile amemweleza Jaji Dkt.Feleshi kuwa,miongoni mwa mambo yanayotisha wanahabari katika sheria iliyopo sasa ni kufungwa bila hata ya yeye (mwanahabari) kuitwa kusikiliza kesi yake.

Jaji Dkt.Feleshi amesema, sheria yoyote lazima ipitiwe vizuri na iwe na uhalali, lakini pia iwe ya wananchi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe.Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amesema, ofisi yake ipo pamoja na hatua zinazochukuliwa na wanahabari katika kuyaendea mabadiliko yanayotakiwa.

"Nipo nanyi na Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) katika hatua ya kuelekea mabadiliko ya sheria za habari,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news