Mwanasheria Mkuu wa Serikali awapa neno viongozi wapya wa TLS

NA DIRAMAKINI

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dkt. Eliezer Feleshi, amewafunda viongozi wapya wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanzania Bara (TLS) ikiwemo kuwapa rai ya kuwa na mifumo bora zaidi ya kiutendaji ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia na kurahisisha ushirikiano kati ya chama hicho na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dk. Eliezer Feleshi akizungumza na Ujumbe wa Baraza la Uongozi wa wapya wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tanzania Bara (TLS) ukiongozwa na Rais wa Chama hicho Prof. Edward Hosea, ulipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma, kujitambulisha na kubadilishana naye mawazo, hivi karibuni. 

AG Jaji Dk. Feleshi ametoa amewafunda na kutoa rai hiyo hivi karibuni, wakati akizungumza na Ujumbe wa Baraza la Uongozi wa TLS ukiongozwa na Rais wa Chama hicho Prof. Edward Hosea, ulipomtembelea Ofisini kwake jijini Dodoma, kujitambulisha na kubadilishana naye mawazo kufuatia uchaguzi wa viongozi wa Chama hicho uliofanyika hivi karibuni.

Katika mazungumzo hayo, Uongozi wa TLS uliwasilisha hoja mbalimbali ambazo walimuomba AG Jaji Dk. Feleshi kuwasaidia kuzifutailia, zikiwa ni pamoja na ombi la kurejeshwa sehemu ya malipo ya wanachama wao zinazolipwa Mahakamani, ombi ambalo walisema kwa msaada wake linaendelea vizuri.

“Nawapongeza kwa kuchaguliwa, wanachama wenu wamewaamini, TLS ni mdau muhimu katika tasnia ya sheria na hususani katika utawala wa sheria, hivyo nawaomba muwe na mifumo mizuri ya kuitendaji ambayo pamoja na mambo mengine itawezesha kubaini mawakili wabobezi katika maeneo mbalimbali ambao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itapenda kuwatumia pale itakapohitaji kufanya hivyo,” akasisitiza AG Dk. Feleshi.

Kuhusu hoja ambazo TLS wameomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusaidia kuzifutalia, AG Feleshi ameahidi kuendelea kuwasaidia kufuatilia kwa baadhi ya hoja ambazo zimo ndani ya mamlaka yake, ikiwamo ya kiwanja, ahadi ambayo aliitoa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha kwa hoja ambazo zipo nje ya mamlaka yake zikiwamo za mabadiliko ya kisheria ili pamoja na mambo mengine, kuongeza muda wa kufanya uchaguzi wa viongozi wa TLS, ameutaka uongozi huo kufuatilia katika Taasisi husika ikiwamo Wizara ya Katiba na Sheria.

AG Dk. Feleshi ameahidi utayari wa Ofisi yake wa kushirikiana na TLS katika kutekeleza majukumu ya kisheria kwa maslahi mapana ya umma wa Watanzania na akawataka TLS kuwa mabalozi na jicho katika utekelezaji wa majukumu hayo.

Kwa upande wao Uongozi TLS, pamoja na mambo mengine ulitumia nafasi hiyo kumpongeza kwa mara nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuteuliwa kwake kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kumshukuru kwa namna ambavyo amekuwa tayari kushirikiana na TLS ikiwa ni pamoja na kusukuma mbele hoja zao mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news