NA JOHN MAPEPELE
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,Mhe.Mohamed Mchengerwa ameitaka Timu ya Soka ya Walemavu ya Tanzania (Tembo Warriors) kutumia mechi za maandalizi na nchi mbalimbali za Ulaya kujinoa ili kushinda kombe hilo na kulirejesha nchini.

“Tumeamua kama Serikali kuendelea kuhahakikisha kuwa tunazisaidia timu zinazofanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa ili kuwasaidia kukuza ajira na kuwafanya waajiriwe kwenye vilabu vikubwa duniani,”amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Amesema, Watanzania wamechoka kuona kuwa nchi inasuasua kwenye michezo na amesisitiza kuwa wakati huu watanzania wanataka Kombe la Dunia kuja Tanzania ambapo amesema hilo litafanikiwa kwa kuweka mbele utaifa na uzalendo wanapokuwa kwenye mashindano haya.

Ameongeza kuwa, jambo kubwa kwa sasa ni kuwa na nidhamu na kuzingatia misingi ambayo wanapewa na makocha wa timu zao ili waweze kufika mbali na kuboresha maisha yao na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa timu hiyo wamemwahidi Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa, wanakwenda kuanza kutema cheche katika maandalizi ya timu hizo za awali ili kujihakikishia kutwa kombe hilo.
Katibu Mkuu, Dkt.Abbasi amesema Tembo Warriors ndiyo timu ya kwanza nchini kufuzu kuingia kwenye mashindano hayo na kuitaka kuendelea kushikilia heshima hiyo kwa kuwa timu ya kwanza kurejesha kombe nyumbani.