NA ASILA TWAHA, OR-TAMISEMI
OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imeshiriki kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani kwa kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wananchi waliotembelea banda la ofisi hiyo.
OR-TAMISEMI ilishiriki Wiki ya Mazingira Duniani kuanzia Juni Mosi, 2022 kwa watumishi wake kupanda miti Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma lengo likiwa ni kutunza mazingira.
Vilevile, OR-TAMISEMI ilishiriki maonesho yaliyoshirikisha wizara, taasisi, wadau wa maendeleo na vikundi mbalimbali vinavyojishughulisha na utoaji wa elimu ya mazingira kwa lengo la kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira ili kuepuka uharibifu wa mazingira nchini.
Kabla ya maadhimisho leo Juni 5, 2022 awali Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alizindua mpango kabambe wa utunzaji wa mazingira na kuzielekeza mamlaka za mikoa na Serikali za Mitaa kuutekeleza na kuhakikisha mpango kabambe wa hifadhi na usimamizi wa mazingira unajumuishwa katika mipango ya bajeti zao.
“Kila Mamlaka za Serikali za Mitaa ihakikishe maeneo yote yaliyoharibiwa yanarejeshwa kwa kupanda miti, inatekeleza vema programu ya Kitaifa ya upandaji wa miti ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya kijani na ihakikishe matukio ya uchomaji ovyo misitu yanadhibitiwa” amesema Mhe. Waziri Mkuu.
Aidha, amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya misitu ya mijini katika Mamlaka zao hayabadilishwi matumizi wa kuvamiwa na kuweka utaratibu wa kuhakikisha taka zinatenganishwa na kukusanywa.
Madhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yalikuwa na kauli mbiu “ TANZANIA NI MOJA TU, TUNZA MAZINGIRA”.