OR-TAMISEMI yatoa maagizo kwa mikoa kuhusu mikopo asilimia 10

NA OR-TAMISEMI

SERIKALI imewataka Makatibu Tawala Mikoa nchini kuhakikisha mafunzo ya mfumo wa mikopo ya asilimia 10 yanafanyika katika ngazi ya halmashauri kabla ya Juni 17, 2022 ili uanze kufanya kazi kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.
Akifunga mafunzo hayo kwa ngazi ya mikoa ambayo yamefanyika jijini Dodoma na kufungwa Juni Mosi, mwaka huu Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI (ELIMU), Dkt.Charles Msonde ameagiza kufanyika kwa mafunzo hayo kwa ufanisi wa hali ya juu.

“Niwatake Makatibu Tawala wa Mikoa wote kuhakikisha kwa vyovyote vile, mafunzo haya mnayoenda kuyasimamia katika ngazi ya halmashauri zetu yanafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu,” amesema Dkt.Msonde.
Amesema, nia ya Serikali ni kuona mfumo huo wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vijana, akina mama na watu wenye ulemavu inakuwa na tija na rahisi kufuatilia, lakini pia inatolewa kwa kuzingatia sheria zilizopo, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo lakini pia inawafikia walengwa wanaotakiwa kupewa ili iwe endelevu.

Aidha, Dkt.Msonde amemwagiza Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuboresha mfumo wa mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri ili iwe rahisi kufanya ufuatiliaji wa madeni ya mikopo na takwimu zote za mikopo kwa kipindi chote cha nyuma.

“Pia nimwagize Mkurugenzi wa TEHAMA Ofisi ya Rais TAMISEMI ahakikishe mfumo huo unaboreshwa zaidi ili uweze kupatana na taarifa za watu waliokopa kule nyuma ili iwe rahisi kufanya ufuatiliaji wa madeni yetu kule nyuma,”amesisitiza Dkt.Msonde.
Naye Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa, Bi.Angelista Kihaga amesema,matarajio ni kuona mfumo wa mikopo ya asilimia 10 utakapoanza kutumika mwezi Julai 2022 unaondoa changamoto ambazo zilikuwa zinakwamisha ufanisi wa utoaji na urejeshwaji wa mikopo hiyo.

“Ni matarajio yetu kuwa mfumo utaendelea kuondoa changamoto za vikundi hewa, kusimamia marejesho, watu kukopeshwa zaidi ya mara moja na changamoto nyingine ambazo zimebaishwa kwa kuwa mfumo huu sasa umeunganishwa na mifumo mingine kama ya NIDA na mfumo wa malipo,” amesema Kihaga.

Aidha, Bi.Kihaga amesema mpaka sasa zaidi ya shilingi Bilioni 100 zimekopeshwa kwa vikundi kwenye halmashauri nchini tangu kuanza kutolewa mapema mwaka 2018/2019.

Kwa upande wake, Anza- Amen Ndossa ambaye ni Mwenyekiti wa Mafunzo ya Vikundi vya asilimia 10 amesema kuwa, mafunzo hayo yamekuja kwa muda mwafaka.

"Mfumo huu utaenda kutatua changamoto kama vile namna ya kupata vikundi vinavyonufaika na mikopo, kujua takwimu sahihi za vikundi katika ngazi zote na kiasi cha fedha kilichokopeshwa,"amesema.

Mafunzo kuhusu Mfumo wa Mikopo ya asilimia 10 yamefanyika jijini Dodoma kwa ngazi ya Mikoa kwa Makatibu Tawala Wasaidizi Mipango, Maafisa TEHAMA na Wasimamizi wa fedha ngazi ya mkoa ambapo kundi la mwisho lilihusisha mikoa ya Geita, Simiyu, Kagera, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mara, Songwe, Dar es Salaam na Morogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Asanteni sana viongozi kwa mfumo bora ila tunasikia tu uku kwetu mwanza pawe kipaombele tunufaike na asilimia kumi

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news