Polisi jino kwa jino dhidi ya wezi, vibaka Lindi

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi mkoani Lindi limewakamata na linawashikilia watu tisa wanaotuhumiwa kufanya kuvunja, kuiba na kuhifadhi mali za wizi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, ACP Mtatiro Kitinkwi amesema watuhumiwa hao wanaoendelea kushikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano walikamatwa katika maeneo na nyakati tofauti ndani ya mwezi Mei, mwaka 2022.

Amesema, jeshi hilo kuanzia Mei 23, 2022 lilianza kufanya msako maalumu katika Manispaa ya Lindi ili kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu. Ndipo lilipofanikiwa kuwakamata watu hao tisa.

Kamanda Kitinkwi amesema, baada ya kufanya mahojiano ya kina baina ya jeshi hilo na watuhumiwa hao walikiri kutenda makosa hayo ya kuvunja na kuiba. Lakini pia baada ya kuwafanyia upekuzi walikutwa na mali zinazo dhaniwa hawakupata kwa njia halali.

Kamanda Kintikwi ambaye hakutaka kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa sababu za kiusalama alitaja mali walizokamatwa nazo kuwa ni TV nane, Redio sita, spika, deki ya runinga, kompyuta mpakato moja, simu mbili aina ya infinex smart na X-Tigi.

Mali nyingine ni kisambaza maji (water dispenser, Hy-pad, simu na sabuni. Huku akiongeza kusema kwamba watuhumiwa hao pia walikamatwa na zana za kuvunjia vitasa, komeo, bawaba na kufuli.

Kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi mkoani Lindi alibainisha kwamba Mei 5,2022 katika mtaa wa Msinjahili, manispaa ya Lindi mmiliki wa baa ndogo inayotambulika kwa jina la GRM Pub, Robert Mosea aligundua ameibiwa runinga mbili na kichanganya sauti za muziki. Mali ambazo zina thamani ya shilingi milioni 4,500,000.

"Baada ya kufanya upelelezi tulibaini kwamba muhusika namba moja wa wizi wa mali hizo ni mlinzi wa pab hiyo ambae alikamatwa tarehe 23.05.2022, kwani tayari alikuwa ametoroka. Alikamatwa wilayani Kilwa eneo la Nangurukuru,"amesema kamanda Kitinkwi.

Mbali na hilo, kamishna msaidizi huyo wa polisi aliongeza kusema kwamba Mei 27,2022 katika manispaa ya Lindi kwa mara nyingine jeshi hilo lilimkamata mtuhumiwa mwingine wa uhalifu, ambaye pia alikiri kushiriki uvunjaji na wizi. Huku akiwataja washirika wake katika kutekeleza mipango ya uhalifu.

"Watuhumiwa watano kati ya hao tisa wanatuhumiwa kuhifadhi na kununua mali za wizi. Wanne wanatuhumiwa kuvunja na kuiba,"Kitinkwi alibainisha.

Alitoa wito kwa wananchi ambao ni raia wema waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kwa kulipatia taarifa za uhalifu na uvunjaji amani. Huku akiweka wazi kwamba msako huo wa kuwasaka wahalifu ni endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news