NA GODFREY NNKO
CHAMA cha Wasioona Tanzania (TLB) Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam kimesema kuwa, wapo tayari kuhesabiwa kupitia Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23,2022.
"Na sisi wasioona, tupo tayari kuhesabiwa kwa maendeleo yetu na Taifa, kwa hiyo Sensa ya Maendeleo na Makazi tunaisubiria na tumeshajiandaa kwa hilo;
Hayo yamesemwa na Katibu wa chama hicho, Wilaya ya Temeke, Bw.Protase Mutakyanga kupitia mahojiano maalum na DIRAMAKINI yaliyofanyika katika ofisi za chama hicho zilizopo Mbagala katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.
Mbali na hayo, Bw.Mutakyanga amesema, wanaandaa mpango wa kufanya mkutano ili kuwahamasisha wanachama wa chama hicho na wananchi wote washiriki kwa ufanisi mkubwa katika zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
"Sisi Chama cha watu wasioona Tanzania, tunatambua kuwa ni sehemu ya wananchi wa Tanzania na ni wajibu wetu kuhesabiwa ili Serikali iweze kuweka sawa mipango yake ya maendeleo.
"Hivyo, kama chama tunaandaa mpango wa kuandaa mkutano ili kuhamasisha wanachama wetu washiriki katika Sensa ya Watu na Makazi na pia kuhamasisha jamii inayokaa na wanachama wetu kuondoa dhana kwamba watu wenye ulemavu ni wa kufichwa ndani.
"Tunazo taarifa za wanajamii ambao wana mtazamo hasi ambao kwanza wao kama wao hawapendi kuhesabiwa, wakiamini kwamba wao ni peke yao wanapaswa kuwatimizia mahitaji yao, jambo ambalo halina ukweli wowote. Ili Serikali iweze kutekeleza mipango yake kwa manufaa ya wananchi inapaswa kufahamu idadi ya watu ambao inapaswa kuwahudumia, na huko ndiko tunakoelekea Agosti 23, 2022." amesema.
Aidha, chama hicho kimetoa ombi kwa wadau mbalimbali nchini wajitokeze kukisaidia fedha shilingi milioni nne kwa ajili ya kuandaa mkutano wa kutoa elimu kwa wanachama wao na jamii kwa ujumla kuongeza ufanisi wa ushiriki katika Sensa ifikapo Agosti 23, mwaka huu.
"Tunaandaa mkutano pale tutakapopata mdau wa kutusaidia kama milioni nne hivi, kusudi tuweze kuandaa mkutano wa wanachama wetu wote ili tuweze kutoa elimu ya namna gani wanachama wetu waweze kushiriki kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi,"amesema Mutakyanga.
Kwa nini Sensa?
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo mwezi Agosti 2022.
Wizara
ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa
kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo
kwenye maandalizi ya kufanya sensa hiyo.
Sensa
ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka
10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.
Hivyo
Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya sita kufanyika nchini baada ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine
zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.
Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na:- Kuisadia
Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa
utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya
afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za
kimataifa;
Taarifa
za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji
wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi
husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali;
Taarifa za msingi za hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote;
Kigawio
katika kukokotoa viashiria vingine mfano Pato la mtu mmoja mmoja, Pato
la Taifa, Ajira na ukosefu wa Ajira na kiwango cha uandikishaji wa
wanafunzi;
Taarifa
itakayowezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo
na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira; na
Msingi
wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia. Takwimu sahihi za Sensa
zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi,
kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa.