NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewaita wafanyabishara kutoka nchini Oman kuja kuwekeza hapa Tanzania.
Wafanyabiashara kutoka Tanzania na Oman pamoja na Wakuu wa Taasisi mbalimbali wakiwa katika Kongamano la Biashara lililofanyika katika eneo la Kasri ya Al Bustan Muscat nchini humo tarehe 13 Juni, 2022.(PICHA NA IKULU).
Mheshimiwa Rais Samia amewahakikishia wafanyabiashara hao mazingira mazuri ya biashara na uwepo wa nguvu kazi ya kutosha.
Wito huo ameutoa Juni 13, 2022 wakati akishiriki Kongamano la Wafanyabiashara nchini Oman ikiwa ni muendeleo wa ziara yake ya kikazi ya siku tatu nchini humo iliyoanza Juni 12, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye Kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman lililofanyika katika eneo la Kasri ya Al Bustan Muscat nchini humo tarehe 13 Juni, 2022.
Amesema, nchini Tanzania kuna fursa nyingi ambazo wawekezaji hao wanaweza kuzitumia katika uwekezaji ikiwemo katika kilimo, uvuvi, madini, utalii na viwanda huku kukiwa na soko la uhakika katika kile watakachokifanya nchini.
Mheshimiwa Rais Samia amesema, endapo Oman itatumia fursa ya kuwekeza nchini Tanzania itanufaika na soko kubwa ambalo Tanzania inaweza kulifikia.
“Sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, pia ni wanachama wa SADC (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika) ambao kwa pamoja tunatengeneza idadi ya watu kuwa karibu ya milioni 500 ambalo ni soko kubwa.Pia sisi ni wanachama wa Soko Huru la Afrika (ACFTA) hili linaongeza idadi ya watu na kufanya soko la watu kuwa 1.3 bilioni," amesema Mheshimiwa Samia.
Pia amesema, Tanzania ni lango la nchi zote za Afrika hivyo mtu anapofanya uwekezaji anaweza kufikia nchi nyingi zaidi kwa wakati mmoja.
Aidha,mbali na soko, Mheshimiwa Rais amesema, kama nchi inayo nguvu kazi ya kutosha huku akieleza kuwa karibu asilimia 67 ya watu wote nchini ni vijana wenye uwezo wa kufanya kazi katika kampuni zitakazoanzishwa na uwekezaji utakaofanywa.
“Pia tumewekeza katika reli ya kisasa ambayo inakatisha katikati ya Tanzania na kuunganisha Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mkifika huko mnaweza kuunganishwa na nchi nyingine za Afrika.,
“Najua kumekuwa na changamoto zinazokatisha tamaa, lakini niko hapa, naenda kufanyia kazi yale yaliyotokea kabla na tunakwenda kufanya kazi pamoja na kufanya uwekezaji kati ya nchi hizi mbili uwe wenye maslahi na manufaa,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.
Mheshimiwa Rais akifafanua baadhi ya maeneo ambayo yanaweza kutumiwa amesema ni lile la ukarimu katika upande wa utalii, kwa nchi kuwekeza katika hoteli kwa kile alichokieleza kuwa licha ya uhitaji wake, lakini bado ni chache.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais amesema kuwa,katika kilimo, uvuvi na ufugaji licha ya sekta hizo kuwa ni muhimu lakini bado hazijaguswa ipasavyo.
Naye Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji nchini Oman, Qais bin Mohammed Al Yousef amesema. wako tayari kujadili ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana na kuendeleza fursa ambazo Tanzania imezitaja.
“Na tupo tayari kuangalia namna tunavyoweza kuimarisha biashara, uwekezaji na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya watu wa nchi zote mbili hususani katika maeneo ya kilimo, uvuvi, viwanda, madini, utalii kama yalivyotajwa na Mheshimiwa Rais Samia,”amesema Waziri huyo.
Tags
Habari
Kimataifa
Kituo cha Uwekezaji Tanzania
Uwekezaji Tanzania
Ziara za Rais Samia Nje na Mafanikio Yake