NA RICHARD BAGOLELE
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Kata ya Bwanga wilayani Chato mkoani Geita kuwa na subira kuhusu urekebishaji wa mipaka ya hifadhi ili kuruhusu sehemu ya ardhi hiyo kutumika katika shughuli za kibinadamu.

Rais Samia ametoa rai hiyo leo wakati akisalimiana na wananchi wa Kata ya Bwanga iliyopo wilayani Chato akiwa njiani kuelekea mkoani Kagera ambapo atakuwa na ziara ya siku tatu.
Katika hatua nyingine Rais Samia amewataka wafugaji wenye mifugo mingi kupunguza idadi ya mifugo hiyo ili kukabiliana na uhaba wa ardhi ambapo amesema iwapo viwanda vingi vya nyama vyama vitaanzishwa kutasaidia kudhibiti ongezeko la mifungo na itasaidia kuuza nyama nje ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule amesema katika kipindi cha muda mfupi mkoa wa Geita umepata shilingi bilioni 190 kwa ajili ya miradi ya elimu, afya, barabara, umeme na maji ambapo kwa upande wa Wilaya ya Chato imeweza kupata shilingi bilioni 22.2 katika miradi ya afya, elimu, maji na barabara.