RC Hapi ataka elimu zaidi kuhusu kodi

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza utoaji wa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara kuhusiana na masuala ya kodi ili waweze kuilipa kwa hiari.
Mheshimiwa Hapi ameeleza hayo wakati wa kikao cha Jukwaa la Wadau wa Kodi la Mkoa wa Mara ambalo limefanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

“Kama tulivyosikia katika majadiliano hapa, wafanyabiashara wanataka wanataka kulipa kodi tatizo wanakosa elimu kuhusiana na aina ya biashara wanayoifanya na kodi wanazotakiwa kulipa” alisema Mheshimiwa Hapi.

Mheshimiwa Hapi ameishauri TRA kuandaa vipeperushi vinavyozungumzia aina za biashara na kodi wanazotakiwa kulipa katika biashara hiyo ili kuwarahisishia wafanyabiashara kuweza kujua kwa wakati wanachotakiwa kulipa kama kodi kwa serikali.

Aidha ameishauri TRA kuunda makundi sogozi (whatsap groups) ya wafanyabiashara wa aina moja ili kuyatumia makundi hayo kubaini kama kuna changamoto na elimu inayohitajika kwa wafanyabiashara wa aina hiyo na kutatua kero zao mara moja.

“Wafanyabiashara wengi hawana elimu ya biashara na kodi, hivyo ili kukusanya kodi kwa utaratibu mzuri TRA inapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu biashara wanazofanya, kodi wanazotakiwa kulipa na matumizi ya kodi hizo katika kuboresha huduma za jamii” alisema Mheshimiwa Hapi.

Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa elimu ya kutosha ikitolewa mara kwa mara itawafanya wananchi kuona fahari katika kulipa kodi n ahata kuwachagua viongozi ambao hawana tabia za kukwepa kulipa kodi kwa serikali.

Aidha ameishauri TRA kufanya utafiti zaidi kuhusu kuongeza wigo wa kodi ili watu wengi zaidi waweze kulipa kodi ili kuongeza mapato ya Serikali na hatimaye serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Hapi amemuagiza Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji Dkt. Noel Komba kuhakikisha Maafisa Biashara wa Halmashauri za Mkoa wa Mara wanawasaidia wafanyabiashara katika kukuza biashara zao kwa kuwapa elimu na ushauri kuhusu biashara zao.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewataka wafanyabiashara kukataa kuwa sehemu ya wafanyabiashara wachache wanaokwepa kulipa kodi halali na kuwataka wakibaini watoe taarifa kwa mamlaka zinazohusika.

Kwa upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Mara Bwana Adam Ntoga ameeleza kuwa majukwaa ya kodi yapo katika mikoa yote Tanzania Bara yenye lengo la kupata mrejesho kutoka kwa wadau wa kodi utakaosaidia kuboresha huduma na kuongeza uhuari wa kulipa kodi.

Bwana Ntoga ameeleza kuwa madhumuni ya kuanzisha baraza hili ni pamoja na kuwezesha majadiliano kati ya TRA na wadau wa kodi ili kuimarisha usimamizi wa kikodi; kushauri juu ya muundo na utekelezaji wa mkakati wa malengo ili kufanikisha dira na dhamira ya mamlaka, kupitia na kuboresha taratibu za kodi ziendane na mazingira ya biashara na kubadilisha mawazo juu ya mifumo ya huduma iliyomo ndani ya mamlaka na kupendekeza namna nzuri ya utoaji wa huduma kwa walipa kodi.

Madhumini mengine ni kutoa maoni na mapendekezo kwenye mpango wa TRA wa kuwaelimisha walipa kodi; kupitia na kupendekeza mabadiliko kwenye sheria na kanuni za kodi, pamoja nan jia za kupambana na ukwepaji wa kodi; kuwasilisha maboresho yoyote yenye lengo la kufanikisha dhumuni la kuanzishwa kwa jukwaa la wadau.

Bwana Ntoga ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria, vikao vya Jukwaa la Wadau wa Kodi vinafanyika mara mbili kwa mwaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news