NA DIRAMAKINI
MKUU wa Mkoa Simiyu, David Kafulila amesema takwimu za ulinganisho wa bei ya umeme Afrika Mashariki zinaonesha kwa wastani Watanzania wanatozwa bei chini ya umeme kuliko nchi zote Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Kafulila amesema hayo leo Juni 1, 2022 kwenye mkutano wa mapokezi ya Katibu Mkuu, Comrade Chongoro wilayani Meatu ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani Simiyu.
"Jana Serikali imetoa bei mpya za mafuta zenye punguzo la takribani shilingi 300 kwa lita kama mkakati wa kupunguza makali ya bei za bidhaa. Serikali itaendelea kuchukua hatua ili kupunguza makali ya gharama za maisha nchini.
"Tuelewe tu kwamba mbali ya mkakati huo kwenye mafuta, pia ni sera ya serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata nishati ya umeme kwa bei nafuu zaidi. Takwimu za ulinganisho wa bei ya nishati ya umeme duniani zinaonesha kwamba wakati bei ya umeme Tanzania wastani ni dola senti 10, Kenya ni dola senti 21, Uganda dola senti 18 na Rwanda ni dola senti 26,"amesema.
"Hii maana yake wananchi wa Kenya wananunua umeme kwa bei kubwa mara mbili ya wananchi wa Tanzania. Na zaidi tunafahamu sera ya serikali kuhakikisha watu wa kipato cha chini kupata nishati ya umeme, kwamba wananchi wanaotumia sio zaidi ya unit 75 kwa mwezi wanalipia unit 1 ya umeme kwa shilingi 100. Yote hii ni namna ya kujenga maendeleo yanayobeba watu wengi,"amesisitiza Kafulila. Pia amewata wananchi kutambua juhudi za serikali katika maisha yao hata kama bado kuna changamoto, kwani serikali inazitambua na kuonekana wazi kukabiliana nazo kwa vitendo.