NA ROTARY HAULE
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewataka maafisa biashara kuwa wabunifu katika utendaji wa kazi zao hususani katika kuibua vyanzo vipya vya mapato.
Kunenge amesema kuwa, Serikali ina matarajio makubwa ya kupata wawekezaji wengi ambao watasaidia kufungua fursa zaidi kwa wawekezaji wengine kuja kuwekeza na kufanya biashara zenye manufaa kwa Taifa.
Kunenge ameyasema hayo Juni 27,2022 Mjini Kibaha wakati akifungua semina ya maafisa biashara kutoka mikoa minne ikiwemo Mkoa wa Pwani, Morogoro, Lindi na Dar es Salaam.
Kunenge amewaambia maafisa hao kuwa uwekezaji unategemea fursa hivyo wanapaswa kubaini fursa zilizopo katika maeneo yao ili kusaidia kuleta wawekezaji sambamba na kuchochea biashara endelevu kwa wananchi.
"Mwekezaji anapokuja nchini kuwekeza atafanya biashara, hivyo lazima nchi yetu itapata kodi, ajira zitaongezeka,na nchi itaweza kupata bidhaa zinazozalishwa ndani na kuuzwa nje ya nchi,"amesema Kunenge.
Amesema kuwa, nchi inataka kuona inafikia matarajio yake lakini kufikiwa kwa matarajio hayo kunategemea zaidi uwepo wa maafisa biashara wanaofanyakazi sehemu mbalimbali hapa nchini.
"Kwa sasa uwepo wenu haupo kwa kiwango cha kutosha ndiyo maana nimesema mafunzo haya ni muhimu sana kwenu hivyo nawaomba mkayatumie mafunzo haya kikamilifu huko katika maeneo yenu,"amesema Kunenge.
Aidha, Kunenge ameongeza kuwa jitihada za serikali kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini zinawahitaji zaidi maafisa biashara na kikubwa kinachotakiwa ni kufanyakazi kwa bidii ikiwa pamoja na kubuni vyanzo vya biashara.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw.Godfrey Nyaisa amesema kuwa,BRELA imeweka mipango madhubuti ya kuhakikisha mfanyabiashara na wawekezaji wanaokuja nchini wanapata huduma kirahisi bila ya usumbufu wowote.
Hata hivyo, Godfrey amewaasa maafisa biashara hao waache kuwa maafisa biashara wa kukaa ofisini pekee na badala yake wawe wabunifu na waache kughushi vitabu vya leseni daraja B.