NA GODFREY NNKO
WAHARIRI wa vyombo mbalimbali vya habari nchini wameoneshwa kuridhishwa kwa namna ambavyo Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula anavyofanya kazi kupitia mfumo shirikishi ambao unawajumuisha wasaidizi wake wote, dhamira ikiwa ni kuifanya Sekta ya Ardhi izidi kuwa neema kwa Watanzania.
Hayo wameyabainisha leo Juni 4, 2022 kupitia kikao kazi cha zaidi ya saa sita kati ya Waziri Dkt.Mabula,Naibu Waziri, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Katibu Mkuu Dkt.Allan Kijazi, Naibu Katibu Mkuu, Nicholas Mserinyo Mkapa, wakurugenzi, makamishina wa ardhi, wakuu wa vitengo na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kilichoketi katika Ukumbi wa Millenium Tower, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Kikao kazi hicho kilionekana cha aina yake ikiwa ni mara ya kwanza Waziri na wasaidizi wake licha ya kukabiliwa na majukumu mengi ya kiserikali kuwapa nafasi wahariri kushauri, kuuliza na kupendekeza namna bora ambayo itawezesha wizara yake kuongeza ufanisi ili iweze kufikia lengo la kutoa huduma bora kwa Watanzania.
Pia kikao kazi hicho kililenga kuwaelezea wahariri mikakati mbalimbali ambayo serikali inayo kupitia wizara hiyo ili kuwa na mtazamo wa pamoja katika kuendeleza sekta hiyo.
Lengo lingine ni kupata mrejesho kutoka kwa wanahabari juu ya changamoto zinazowakabili na kupata ushauri wa wao jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo ili kujenga mazingira mazuri ya kuhakikisha kwamba kila mtanzania anafaidika na ardhi ya nchi yake na pia anapata haki yake kutokana na misingi ya sera, sheria kanuni na taratibu zilizopo.
Awali
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Deodatus Balile amesema kuwa, wizara ya ardhi imebeba dhamana kubwa kwa Watanzania, hivyo anaamini ushirikiano huu ulioanza baina ya wizara na wanahabari ni daraja muhimu sana.
"Wizara ya Ardhi ni wizara nyeti ambayo inagusa maisha ya kila Mtanzania...tunaamini kwamba upele umepata mkunaji, tukiamini kwamba sasa mtakwenda kijidigitali, migogoro ambayo imeleta utengano katika familia au jamii mtaitafutia ufumbuzi kidigitali kwa sababu sasa hivi tunakwenda kwenye digital economy. Tunashukuru sana kwa ushirikiano huu," amesema
Katibu Mkuu
Katibu Mkuu, Dkt.Allan Kijazi amesema kuwa, "Siku ya leo tumekutana kubadilishana mawazo kuhusu mafanikio, changamoto na mikakati ambayo ipo katika kusimamia sekta ya ardhi katika nchi yetu.
"Kama ambavyo amesema Mwenyekiti Sekta ya aAdhi ni sekta muhimu sana kwa kila mtanzania haijalishi cheo chako, haijalishi uwezo wako wa kiuchumi, haijalishi unaishi mjini au kijijini kila mtanzania utakayemgusa lazima anaathirika na maamuzi mbalimbali yanayotolewa kuhusu sekta ya ardhi kwa sababu ndio tegemeo na msingi wa maendeleo katika nchi yetu,"amesema Dkt.Kijazi
"Kama mnakumbuka Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema ili tuendelee tunahitaji mambo manne kw amaana ya Watu, Ardhi, Siasa safi na Uongozi bora kwa hiyo wizara hii imekabidhiwa jukumu kusimamia Sekta ya Ardhi mojawapo ya misingi minne mkuu ya Maendeleo Katika nchi yetu.
"Kama ni Msingi mkuu wa Maendeleo katika nchi yetu hatuwezi kuwa mbali na wananchi, lakini pia hatuwezi kumfikia kila mwananchi mmoja mmoja lazima tuwe na utaratibu kwanza kujua wananchi wanasema nini lakini pili kuwapa mrejesho wa mikakati mbalimbali ambayo serikali inayo kupitia Wizara ya Ardhi ili kuweza kuwa pamoja na kuwa na mtazamo wa pamoja wa jinsi ya kuendeleza sekta hii,"amesema na kuongeza.
"Wakati wa utambulisho nimeeleza wazi kwamba ipo migogoro inayoendelea na sisi kama wizara hatutaki kuona migogoro hiyo inaendelea, lakini unakuta kwamba baadhi ya migogoro aidha unakuta kumekuwa na changamoto za kiutendaji ndizo zimesababisha migogoro, lakini kingine tumekiona wakati mwingine migogoro inaibuka kutokana na wananchi kuwa na uelewa mdogo kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazohusu masuala ya ardhi.
"Na kutokana na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu hizo sheria basi wale wenye uelewa wa sheria na wakati mwingine wenye uwezo wa kiuchumi wanatumia uelewa mdogo wa wananchi kuweza kuwakandamiza au kukandamiza haki zao".
Ushirikiano
"Tukaona kwamba ni vizuri basi kutokana na hali hii sisi kama Wizara tujenge ushirikiano na wenzetu wa Sekta ya Habari kwa sababu ninyi mnalo jicho kila mahali mnajua nini kinachoendelea wakati mwingie wananchi wanakuja kwenu, wakati mwingie mnatoa taarifa, lakini taarifa hizo wakati mwingine unakuta zinapotoshwa kwa hiyo katika kikao hiki pamoja na masuala mengine kutakuwa na wasilisho ambalo linalenga kuelimishana kujusu sera, sheria, kanuni na taratibu zilizopo,"amesema.
"Ili kwanza ninyi wenyewe miweze kujenga uelewa, lakini baada ya kujengewa huo uelewa, kazi inayofuata sasa itakuwa ni kushirikiana kuweza kuwaelimisha wananchi ili waweze kufahamu haki na wajibu wao katika masuala ya usimamizi wa sekta ya ardhi.
"Hivyo ni imani yangu kwamba, mtakuwa washiriki wazuri kusikiliza kitakachowasilishwa, lakini pia kutoa maoni yenu na baada ya hapo kutupa ushauri wa namna bora ambavyo tunaweza tukashirikiana ili kuendelea kuwajengea ninyi wenyewe uelewa wa masuala mbalimbali yanayohusu masuala ya ardhi na jinsi mtakavyoshiriki kuwaelimisha Watanzania ili kila mmoja ajione anayo haki na fursa kama mtanzania mwingine yeyote bila kujali anaishi wapi na anatoka wapi,"amefafanua Dkt.Kijazi.
Ongezeko la Watu
"Na hili ni muhimu kwa muda huu tulionao ambapo kama mnavyofahamu idadi ya Watanzania inazidi kuongezeka, lakini ardhi haiongezeki.
"Kwa hiyo huko tunakokwenda tusipojipanga vizuri tutajijuta tumeingia kwenye migogoro isiyoisha ambayo itazorotesha shughuli za kiuchumi, shughuli za kijamii na itazorotesha mikakati mbalimbali ya uhifadhi wa masuala ya mazingira kama mnakumbuka vizuri huko nyuma tulikuwa Watanzania karibu milioni 10 lakini sasa hivi tuko kati ya milioni 60 na milioni 70.
"Na taifiti zilizofanyika zinaonesha itakapofika mwaka 2100 Watanzania tutakuwa tumeongezeka tumefikia milioni 275 sijui kama hilo mnalifahamu? Lakini kwa trends (mwenendo) tuliyonayo wa kuzaana ili tuujaze ulimwengu ndio hiyo tutakuja kuishia huko kuwa Watanzania milioni 275,"amesema Dkt.Kijazi
"Itakapofika mwaka 2100 sasa leo hii tuko Watanzania milioni 70 hali ni hii, hebu imagine (fikiri) itakapo fika hiyo ya Watanzania milioni 275 hali itakuwaje, na mara nyingi tumekuwa tukisema hao watakaokuja watajua wenyewe, lakini hao watakaokuja tujue ni watoto wetu na ni wajukuu wetu sisi tunaandaa mazingira gani ya kuhakikisha kwamba tunazuia crisis (migogoro) kwa miaka inayokuja," amesama.
Dar inaongezeka
"Sasa hivi Dar es Salaam tunakisiwa tuko milioni 6 au milioni 7, lakini itakapofika mwaka 2035 Dar es Salaam inakisiwa itakuwa na wakazi milioni 14 fikiria mwaka 2035 ni miaka 13 tu kutoka mwaka huu tulionao na hao watakaokuja ukibahatika kuwepo sasa hivi tuko milioni 6 au milioni 7 tukifika milioni 14 itakuwaje kama tusipojipanga sasa hivi.
"Sasa tuelewe kwamba hili jukumu pamoja na kwamba Wizara ya Ardhi inalo jukumu la kusimamia sekta hii ya ardhi, lakini ni kukumu la kila mtanzania aelewe kwamba analo jukumu la kutoa mchango wake kwa kuhakikisha kwamba tunayo mikakati sahihi ya kusimamia sekta hii, lakini tunaweka utaratibu mzuri wa kutatua migogoro,"amesema.
"Na tunategemea kwamba maoni yatakayotolewa yatatusaidia kuboresha sera zetu, sheria zetu, na mikakati yetu ili tuweze kuzuia changamoto ambazo zinaweza kujitokeza kwa watoto wetu na wajukuu wetu na wale ambao watakaobahatika kuwepo kwa hiyo nimalizie kusema kwamba lengo kuu tunayo malengo makuu matatu ya kikao chetu.
"Lengo la kwanza ni kujengeana uwezo au uelewa wa mikakati ya Serikali katika kusimamia sekta ya ardhi kwa hiyo kuweni huru kutoa michango yenu kukosoa na kushauri namna bora ambayo tunaweza kuboresha.
"La pili, kufanya tafakari ya pamoja jinsi ambavyo tunaweza kushirikiana kuondoa changamoto mbalimbali ambazo zinatukabili na ambazo zitatukabili kwenye miaka ijayo tusipojipanga vizuri, na lengo la tatu kukubaliana namna bora ya kushirikiana ili tuwe na mkakati endelevu wa kuweza kutoa elimu kwa wananchi.
"Lakini pia kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi ili tuweze kuwa na mikakati ambayo ni endelevu na nina imani tukifanya hivi tutaachana na utamaduni wa kuripoti tukio moja moja tu,likitokea tukio moja utakuta tunang'ang'ana na hilo wakati kuna masuala mengine ya msingi, tunapaswa kuyaangalia kwa upana wake kabla ya kujikita kwenye tukio moja moja,"amefafanua kwa kina Dkt.Kijazi.
Waziri amesemaje?
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula wakati akifungua kikao kazi hicho amesema kuwa, Mkoa wa Dar es Salaam umekithiri kwa uvamizi wa ardhi hasa kwa baadhi ya wananchi kununua maeneo na kuyaendeleza bila kujua uhalali wa umiliki wa eneo husika.
“Hali ya uvamizi wa ardhi kwa Mkoa wa Dar es Salaam imekithiri kwa kiasi kikubwa, watu wana hati za umiliki wa maeneo lakini hawataki kuendeleza maeneo hayo.Wanatokea wajanja wanauza eneo hilo kwa mtu mwingine ambaye haulizi uhalali wa eneo hilo kwa ofisi husika anajenga kumbe amevamia eneo la mtu,"amesema.
Waziri Dkt. Mabula amesema kuwa, ni vyema wananchi wakazitumia ofisini za ardhi zilizopo kote nchini wakitaka kujenga au kuendeleza maeneo kabla ya kukumbana na kadhia ya uvamizi pindi sheria inapofuata mkondo wake.
“Wananchi wasifikiri wakivamia maeneo ya watu watarasimishiwa maeneo hayo, ukivamia eneo sheria ikafuata mkondo wake kilio kisirudi kwetu…nitoe rai, mjiridhishe kabla ya kufanya endelezaji wa maeneo hayo,”amesema Waziri Dkt.Mabula.
Pia amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi Bilioni 50 kwa wizara hiyo ambazo zimeelekezwa kwa halmashauri 55 katika mradi wa KKK (Kupanga, Kupima na Kumilikisha) kwa kasi maeneo, mradi huo unashirikisha Serikali na taasisi binafsi katika kuhakikisha jamii pia inapata uelewa kuhusiana na umiliki wa ardhi na umuhimu wa upangaji wa miji.
"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa fedha zilizoelekezwa katika halmashauri 55, baada ya Royal Tour nchi zote zinaitazama Tanzania wizara imejipanga hatutamwangusha Rais katika kasi yake ya kuifungua nchi na tukiwa kiungo muhimu kwa nchi na uchumi katika uwekezaji, kilimo, mifugo na miundombinu tumetenga maeneo ya kutosha katika miji 27 tayari kwa kuwapokea wawekezaji,”amesema Waziri Dkt.Mabula.
Pia amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imeendelea kufanya maboresho katika sekta hii kwa kutunga na kusimamia Sera na Sheria mbalimbali.
Vilevile, kuandaa kanuni, miongozo, kuratibu utekelezaji wa mikakati mbalimbali ndani ya sekta ikiwa ni lengo la kuhakikisha upatikanaji wa milki salama za ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Aidha, Waziri Dkt.Mabula amesema sekta ya ardhi imeendelea kuwa kiungo wezeshi kwa sekta nyingine za uzalishaji zikiwemo; Viwanda, Kilimo, Mifugo na Miundombinu.
"Mwelekeo wa Wizara ni kuwa na mfumo wa kidigitali. Wizara inaendelea kuhuisha kumbukumbu za wamiliki wa ardhi katika mifumo ya TEHAMA na kuendelea na zoezi la uhakiki wa taarifa za wamiliki kupitia zoezi la ubadilishaji wa nyaraka za umiliki (data conversion) kutoka analojia kwenda digitali na utambuzi wa maeneo yasiyopimwa,"amesema Dkt.Mabula.
HABARI HII INAENDELEA CHAPISHO LIJALO HAPA DIRAMAKINI, USIKOSE