Serikali yazifanyia kazi hoja 13 za madereva, wamiliki vyombo vya usafirishaji

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imezishughulikia hoja na malalamiko takribani 13 kutoka kwa Madereva na Wamiliki wa vyombo vya Usafirishaji nchini, baada ya wadau hao wa sekta ya usafirishaji nchini kuwasilisha masuala hayo, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akiongea na Waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kushughulikia hoja na malalamiko takribani 13 kutoka kwa Madereva na Wamiliki wa vyombo vya Usafirishaji nchini Jijini Dodoma Juni 11, 2022. (Picha na OWM).

Katika kuimarisha ustawi wa sekta hiyo ili iweze kukuza uchumi wa Taifa, Ofisi hiyo ilikutana na wadau hao kwa nyakati tofauti na kujadili namna bora ya kuzipatia ufumbuzi hoja na malalamiko hususani ya mikataba, mishahara, Posho za safari, Bima ya Afya, Pensheni, Matumizi ya Speed Governor, Usafirishaji wa sumu, mafuta na gesi, Ukaguzi wa magari na magari kuingia vituo vya mabasi. 

Akiongea na Waandishi wa habari Jijini Dodoma Juni 11, 2022. Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi, amesema dhamira ya serikali ni kujenga mazingira wezeshi kwa wadau wote wa sekta hiyo wakiwemo madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji. 

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na wadau sekta ya usafirishaji nchini kwa kuhakikisha kero na changamoto zinazoikabili sekta hii zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu,” amesisitiza Katambi. 

Amefafanua kuwa hoja zote zilizowasilishwa zimefanyiwa kazi kwa kukubaliana katika vikao vya pamoja, ikiwemo Viongozi wa Vyama vya Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji wameahidi kutoa mikataba ya kazi kwa madereva kwa kuzingatia rasimu ya mkataba wa ajira ulioandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau. 

Amefafanua kuwa kuhusu mishahara ya madereva kupitia Benki, Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji wapo tayari kutekeleza jambo hili. Aidha, Serikali inawashauri madereva kufanya makubaliano na waajiri wao kuhusu suala hili kwa kuzingatia Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini. 

Ameongeza kuwa, Serikali imewaelekeza Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji wahakikishe ifikapo tarehe 30 Julai, 2022 kuwasajili wafanyakazi wao wote katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF na WCF) wakiwemo madereva. Pensheni kwa Wastaafu na kuwasilisha michango yao kwa wakati 

Mhe,Katambi amebainisha kuwa suala la Bima ya afya, kwa kuwa ni suala la makubaliano, wamiliki wapo tayari kukubaliana na madereva kuhusu utekelezaji wake. 

Amesisitiza kuwa, Suala la matumizi ya Speed Governor badala ya VTS, Wamiliki nao wana mtazamo sawa na madereva kuhusu changamoto za matumizi ya VTS, hivyo serikali imetoa maelekezo kwa mamlaka zinazohusika kulifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na wadau wa sekta husika. 

Suala jingine lililofanyiwa kazi ni Kuhusu posho za safari za ndani na nje ya nchi na Mileage za safari, ambapo Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji wamepokea hoja hii na wameahidi kuendelea kufanya Majadiliano ya Pamoja na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva na kufunga Mkataba wa Hali Bora kwa lengo la kuboresha posho na maslahi mengine ya Madereva, kwa kuzingatia utofauti uliopo baina ya mwajiri mmoja na mwingine. 

Aidha, amefafanua kuwa; utaratibu wa kupakia na kushusha mafuta na gesi, Wamiliki wa Vyombo vya usafirishaji wamebainisha kuwa elimu inaendelea kutolewa kwa madereva ili kuwapa uelewa wa namna suala hili linavyosimamiwa. Aidha, Serikali imeelekeza mamlaka zinazohusika kulifanyia kazi kwa kushirikaina na wadau na kwa kuzingatia muda uliopangwa. 

Masuala mengine ni; Kuhusu utaratibu wa kusafirisha sumu, Wamiliki wa Vyombo vya usafirishaji wanao mtazamo kuwa Sulphur sio sumu. Hata hivyo, Serikali imeelekeza mamlaka husika ifanyie kazi hoja hiyo ili kujiridhisha na ukweli wake kwa lengo la kuiwezesha kuchukua hatua stahiki. Sehemu ya Wakuu wa Idara kutoka ofisi hiyo wakifuatilia maelezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (hayupo pichani). 

Mhe. Katambi ameongeza kuwa, Serikali inaendelea na zoezi la kufanya Kaguzi Jumuishi (Joint Inspection) za wadau wanaoguswa na sekta hii hadi mwezi Agosti. Aidha, serikali imekubaliana na Wamiliki wa Vyombo vya usafirishaji kuwa Jeshi la Polisi liendelea kusimamia ukaguzi wa magari ili kuhakikisha magari mabovu hayaruhusiwi kufanya safari ndani na nje ya nchi na hatua kali ziendelee kuchukuliwa kwa wamiliki watakaobainika kutumia magari mabovu. 

Hatua nyingine ni serikali wamekubali kuanzisha Kanzi Data ya Madereva ambapo Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji wameona umuhimu wa hoja hii, hivyo, wameiomba Serikali iharakishe ukamilishwaji wa Kanzi Data hiyo. 

Serikali imekubaliana na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji kuhusu wafanyakazi wake kujiunga na vyama vya wafanyakazi, hivyo kwa kuwa ni suala la hiari kwa wafanyakazi na pia ni moja ya haki zao za msingi kwa mujibu wa Sheria. Hivyo, wameviomba Vyama vya Wafanyakazi kuwahamasisha Madereva kujiunga na Vyama hivyo na kuhakikisha wanaunda Matawi katika Maeneo ya Kazi. 

Suala la mabasi ya abiria kuingia kila kituo kwa safari za mikoani, Serikali inaendalea kulifanyia suala hili kwa kuzingatia taratibu zilizopo na kwa kuzingatia mazingira ya ufanyaji hivyo wanaendelea kushirikiana na wamiliki wa vyombo vya Usafirishaji ili kulipatia ufumbuzi wa kudumu. 

Kuhusu kutotimiza wajibu wao; Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji wameona umuhimu wa kuwa na Maafisa Rasilimali Watu katika maeneo yao ya kazi. Aidha, watahakikisha wanawapa elimu ya Sheria za Kazi na kuhakikisha wanakuwa na Sera za Ajira. 

Halikadhalika, Naibu Waziri Katambi amewasihi Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kuzingatia utaratibu uliowekwa kisheria katika kuitisha migomo ya wafanyakazi. Hivyo amesisitiza kuwa Serikali itaandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa Waajiri wote wa Sekta ya Usafirishaji ili kukuza uelewa kwa Maafisa Rasilimali Watu na Maafisa Mahusiano ili watimize wajibu wao kwa tija ya sekta hiyo. 

Aidha, alitoa wito kwa Madereva wasio wanachama wa Vyama vya wafanyakazi kuacha kutumia njia zisizo halali kisheria kuanzisha ama kuchochea migomo kwani kufanya hivyo ni uvunjifu wa Sheria za nchi. Hivyo,serikali itaendelea kuitisha vikao vya mashauriano ya wadau, kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kawaida bila kusubiri kuibuka kwa migogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news