SHUKRANI SERIKALI:Ile bilioni mia, makali yamepunguka, Bei mafuta sikia

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na ongezeko kubwa la bei ya mafuta nchini.
Bei za mafuta, kwa muda katika soko la Dunia zimeongezeka kwa kasi kutokana na sababu mbalimbali, moja wapo ikiwa ni vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, vita ambavyo vilianza mwishoni mwa mwezi Februari, mwaka huu.

Vita hivyo, vimesababisha kuharibika kwa mfumo wa usambazaji wa mafuta duniani kutokana na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi, sababu iliyochangia mafuta ghafi kupanda bei.

Kwa mfano, mwezi Machi, mwaka huu bei ya pipa ilikuwa inacheza kuanzia dola za Marekani 60.3 hadi dola za Marekani 139.13 kwa pipa, gharama ambazo zimechangia soko la ndani bei kuwa juu.

Licha ya changamoto hiyo, Serikali imekuwa ikitumia kila njia kuhakikisha inadhibiti bei ya nishati hiyo ili kuwapunguzia wananchi makali na kuhakikisha kunakuwepo mafuta ya kutosha muda wote.

Ndiyo maana, mwezi Mei, mwaka huu Mheshimiwa Rais Samia alitoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 katika harakati za kukabiliana na ongezeko la bei za mafuta katika soko la ndani kwa mwezi huu wa Juni, lakini kwa upekee, Mheshimiwa Rais akiwa ziarani mkoani Kagera amesema, ruzuku hiyo itaendelea kutolewa kila mwezi ili kutoa nafuu zaidi ya bei ya mafuta.

Ungana na mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande hatua kwa hatua uweze kujifunza jambo kupitia shairi lifuatalo hapa chini kuhusu uamuzi huu wa hekima kutoka kwa Rais Samia;

1).Ile bilioni mia, makali yamepunguka,
Bei mafuta sikia, angalau yashikika,
Nyuma haijafikia, kidogo tunaridhika,
Shukrani serikali, hili lililofanyika.

2).Mafuta tunatumia, kwingi tukiwajibika,
Bei kama zazidia, matatizo yaumuka,
Kote yaingia, kutuletea mashaka,
Shukrani Serikali, hili lililofanyika.

3).Bila ya kuingilia, bei kubwa kuishika,
Tungezidisha kulia, kwa bei kutoshikika,
Vingi tunavyotumia, ngeshindwa kununulika,
Shukrani Serikali, hili lililofanyika.

4).Hali tunayopitia, sote tunalalamika,
Kwetu haijaanzia, ya kwamba tunaitaka,
Ukraine na Russia, vita vyao vyahusika,
Shukrani Serikali, hili lililofanyika.

5).Fedha ilizotumia, kwa makali kupunguka,
Huko ni kuingilia, mengine yalopangika,
Bado twaiamia, tulipo twaweza vuka,
Shukrani Serikali, hili lililofanyika.

6).Tena tunafurahia, Rais amesikika,
Hali tunayopitia, hatutabaki kuchoka,
Nafuu kutupatia, itazidi kufanyika,
Shukrani Serikali, hili lililofanyika.

7).Mafuta yakumbushia, mengi ya kufikirika,
Vipi twaweza tumia, zizotufika baraka,
Gesi yetu asilia, endapo tungeiteka,
Shukrani Serikali, hili lililofanyika.

8).Wito tunatoa pia, kwenyewe uweze fika,
Wanotuunganishia, ili gesi kutumika,
Bei ngetupunguzia, magari ngeongezeka,
Shukrani Serikali, hili lililofanyika.

9).Gesi tunaisikia, magari ikatumika,
Lakini kuifikia, bei kuunga ni shaka,
Kimyakimya twabakia, bei mafuta kushika,
Shukrani Serikali, hili lililofanyika.

10).Mioyoni yabakia, kuhimiza wahusika,
Vita yao ngeishia, tuweze kupumzika,
Bei zilipofikia, ili zizidi kushuka,
Shukrani Serikali, hili lililofanyika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news