NA DIRAMAKINI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imepata hati safi kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Pia Halmashauri hiyo imefunga hoja 31 kati ya hoja 41 baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakiki na kuridhia majibu yaliyowasilishwa na kufanya hoja zisizofungwa kuwa 10.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Samwel Warioba ameyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya CAG ya mwaka 2020/2021.
Warioba amesema kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 na vipindi vya nyuma halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 41 na hoja 24 ziliibuliwa na kutolewa mapendekezo katika mwaka 2020/2021 pekee.
Hata hivyo, amesema hoja nne za mwaka 2020/2021 na hoja sita za miaka ya nyuma, mkaguzi hajaridhia kuzifunga kutokana na baadhi ya hizo kuwa za kimfumo na kiutendaji.
"Kwa miaka ya nyuma hoja ambazo CAG alikuwa hajaridhia kuzifunga ni 17 ikihusisha hoja za miaka ya kuanzia 2014/2015 hadi 2019/2020," amesema Warioba.
Amesema jumla ya hoja 10 ambazo hazijafungwa, utekelezaji wa hoja zilizobaki unaendelea kwa matarajio kuwa zitafanyiwa ufumbuzi baada ya kikao na majibu na vielelezo vyake vitawasilishwa kwa wakaguzi mwakani.
"Ofisi ya mkurugenzi inapenda kutoa shukurani za dhati kwa Mwenyekiti wa halmashauri, mbunge na madiwani kwa uratibu, ushauri na maelekezo ya mara kwa mara hadi ofisi ya CAG kutoa hati safi," amesema Warioba.
Mkuu wa mkoa wa Manyara,Makongoro Nyerere, pamoja na kuwapongeza kwa kupata hati safi ameiagiza halmashauri hiyo kumaliza hoja zilizopo.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt.Suleiman Serera, amesema kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza zinapaswa kumalizwa Kwa utaratibu maalum.