NA MWANDISHI WETU
TANZANIA na Umoja wa Ulaya zimeazimia kuongeza ushirikiano katika ubia wa maendeleo na kutumia mpango wa umoja huo wa Global Gateway Investment Package kuchochea uwekezaji nchini kupitia uchumi wa buluu, kilimo, usafiri, nishati na digitali.
Maafikiano hayo yamefanyika baina ya Mkurugenzi Mkuu wa Ubia wa Kimataifa (International Partnership) wa Umoja wa Ulaya, Bw. Koen Doens na Balozi wa Tanzania Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Nyamanga walipokutana kwa mazungumzo yaliyofanyika tarehe 20 Juni 2022 makao makuu ya Umoja wa Ulaya Jijini Brussels nchini Ubelgiji.
Bw. Doens amepongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake katika kufanya mageuzi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na kuongeza kuwa umoja huo unaridhishwa na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita za kuwaletea maendeleo wananchi wake ambazo ni muhimu katika ustawi wa jamii, kujenga umoja wa kitaifa na kuvutia wawekezaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiongozana na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU) Charles Michel, baada ya kuwasili Makao Makuu ya Baraza hilo Brussels nchini Ubelgiji, Februari 15, 2022. (Picha na Ikulu).
Amesema Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Tanzania kutekeleza miradi
itakayokubaliwa chini ya Mpango wa EU-Africa Global Investment Package uliotengewa kiasi cha Euro bilioni 150 ambapo katika kipindi cha miaka saba ijayo umepanga kuipatia Tanzania misaada ya kiasi cha Euro milioni 703 sawa na shilingi Trioni 1.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kiasi hiki kimejumuisha nyongeza ya Euro milioni 277 kutoka Euro milioni 426 zilizotangazwa kutolewa awali na Umoja huo wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya mwezi Februari 2022.
Balozi Nyamanga amemhakikishia Bw. Koen Doens kuwa Tanzania inathamini uhusiano uliopo na ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa misaada ya maendeleo ambayo imekuwa ikiipatia Tanzania tangu mwaka 1975 ulipoanza ushirikiano huo.