Tanzania yapata tuzo Maonesho ya 37 ya Utalii Korea Kusini

NA DIRAMAKINI

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imepata tuzo kwa kuwa na banda bora lenye ubunifu wa kutangaza utalii katika Maonesho ya 37 ya Utalii ya Seoul International Travel Fair (SITF).
Balozi wa Tanzania nchini Korea, Balozi Togolani Mavura akipokea tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Maandalizi ya maonesho ya SITF, Shin Joong-mok.

Hayo yamesemwa na Balozi wa Tanzania nchini Korea, Mhe. Balozi Togolani Edriss Mavura wakati akikabidhiwa tuzo hiyo na Mwenyekiti wa Maandalizi ya Maonesho ya SITF, Mhe. Shin Joong-mok. Makabidhiano hayo yalifanyika katika banda la Tanzania.

Maonesho hayo yalifanyika katika jiji la Seoul nchini Korea Kusini kuanzia tarehe 23 hadi 26 Juni, 2022.

Balozi Togolani amesema,tuzo hii ni ishara nzuri ya ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wadau wa utalii wa Tanzania katika kuandaa ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya SITF.

"Tutaendelea kuzijongea fursa za kutangaza utalii wa Tanzania na kushiriki katika matukio mbalimbali yatayofanyika hapa Korea,"amesema.

Banda la Tanzania lilipambwa kwa kuonesha vivutio mbalimbali vinavyopatikana nchini Tanzania ambapo picha za Utalii wa kutamaduni, Mlima Kilimanjaro, fukwe za Zanzibar, nyumbu wanaovuka Mto Mara, na madini ya Tanzanite zimewavutia wageni wengi waliotembelea maonesho hayo.

Katika Banda la Tanzania wananchi wa Korea waliweza kujitokeza kwa wingi kunywa na kufurahia ladha ya kahawa ya Tanzania. Tukio hilo lilichangia Banda la Tanzania kutembelewa na wageni wengi.

Kahawa iliyotumika kwenye maonesho haya ni ile inayolimwa katika wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.

Aidha, wanawake wengi waliotembelea banda la Tanzania walivutiwa sana na ususi wa nywele ambapo walijitokeza kwa wingi kusuka nywele zao. Jambo ambalo walionesha kulifurahia sana.

Kwa upande wa Bodi ya Utalii Tanzania, Afisa Habari na Uhusiano,Augustina Makoye amesema wanaendelea kubuni njia mbalimbali za kutangaza utalii wa Tanzania ili vivutio vya Tanzania viweze kujulikana zaidi katika soko hili ambalo wananchi wengi wameonesha kuvutiwa zaidi na vitu vya kiutamaduni.

Amesema, wataendelea kuliwekea mkakati wa kutangaza utalii wa kiutamaduni kwa vitendo ili tuweze kuwavutia watalii wengi kutoka Korea Kusini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news